×

Taifa Group Yatoa Tahadhari Jukwaa Feki la Uwekezaji ‘TaifaAI’

TAIFA Group imewaonya wananchi kuhusu jukwaa feki la uwekezaji linalotumia jina “TaifaAI”, likidai kuhusishwa na mfanyabiashara Rostam Aziz na Taifa Group.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 4, 2026, Taifa Group imesema maudhui kuhusu jukwaa hilo yanasambazwa kupitia Facebook, Instagram na mitandao mingine ya kijamii, yakitumia jina, picha na utambulisho wa Rostam Aziz pamoja na Taifa Group.

Taifa Group imekanusha kuwa na uhusiano wowote na “TaifaAI”, ikisisitiza kuwa Rostam Aziz hajaanzisha, hajaidhinisha wala kulitangaza jukwaa hilo.

Kampuni hiyo imewaonya wananchi wasijiandikishe, wasitoe taarifa binafsi au za benki, wasitume fedha na wasifanye miamala na watu wanaodai kuiwakilisha “TaifaAI” au Taifa Group.

Aidha, Taifa Group imesema Rostam Aziz hatumii jina au nafasi yake kuhamasisha wananchi kujiunga na miradi ya uwekezaji au mifumo ya biashara mtandaoni inayowaahidi faida za haraka za kifedha.

Kampuni hiyo imeeleza kuwa inachukua hatua kwa kuwasilisha taarifa za utapeli huo kwa mamlaka husika pamoja na watoa huduma wa mitandao ambako maudhui hayo yanasambazwa.

Taifa Group imewasihi wananchi kuwa waangalifu na kutegemea njia rasmi za mawasiliano za kampuni hiyo pekee kupata taarifa kuhusu shughuli zake.

Taarifa hii imetolewa na Taifa Group, Septemba 4, 2026.

Leave a Comment