×

Mtangazaji TV Ahukumiwa Kunyongwa Pamoja na Washtakiwa Wengine 11

CAIRO, Misri — Mtangazaji na mtayarishaji wa vipindi vya televisheni nchini Misri, Sarah Khalifa, mwenye umri wa miaka 39, amehukumiwa kifo kwa kunyongwa pamoja na washtakiwa wengine 11 katika kesi kubwa ya dawa za kulevya iliyofikishwa katika Mahakama ya Jinai ya Cairo.

Khalifa anafahamika zaidi kwa kuendesha kipindi cha televisheni “Mission Impossible”, kilichokuwa kikijikita katika masuala ya uhalifu na usalama.

Kwa mujibu wa taarifa za mahakama, Khalifa na washtakiwa wenzake walipatikana na hatia ya kuunda mtandao wa uhalifu uliopangwa, uliodaiwa kujihusisha na uingizaji wa malighafi zilizotumika kutengeneza dawa za kulevya kwa ajili ya biashara.

Washtakiwa hao pia walikabiliwa na makosa mengine yanayohusiana na umiliki wa silaha na risasi bila leseni.

Mamlaka nchini humo ziliripoti kuwa wakati wa uchunguzi wa kesi hiyo, zilikamata zaidi ya kilo 750 za dawa za kulevya na malighafi, huku maeneo mawili yakidaiwa kutumika kama maabara za kutengeneza dawa hizo.

Kesi hiyo ilikuwa na washtakiwa 28 kwa jumla. Kati yao, watu 12 wamehukumiwa kifo, huku wengine tisa wakihukumiwa kifungo cha maisha na saba kuachiwa huru.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya mahakama kupata maoni ya Mufti Mkuu wa Misri, hatua inayohitajika katika kesi zinazoweza kupelekea hukumu ya kifo nchini humo.

Hata hivyo, hukumu hiyo bado inaweza kukatiwa rufaa kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

Sarah Khalifa amekuwa akikanusha kuhusika na tuhuma hizo. Wakati wa kutolewa kwa hukumu hiyo, mtangazaji huyo aliendelea kusisitiza kuwa hana hatia.

STORI NA TEREZA MUGA | GPL-TUDACO

Leave a Comment