×

Dkt. Mwinyi Atoa Pole kwa Rais Samia Kufuatia Kifo cha Mumewe, Kuzikwa Leo Kizimkazi, Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia kifo cha mume wake, Marehemu Hafidh Ameir Hassan.

Marehemu Hafidh Ameir Hassan amefariki dunia leo, Septemba 7, 2026, katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Zanzibar.

Katika salamu hizo, Rais Dkt. Mwinyi amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo na kuungana na Rais Dkt. Samia, familia, ndugu, jamaa pamoja na wote waliofikwa na msiba huo katika kipindi hiki cha majonzi.

Amesema kifo hicho ni pigo kubwa kwa familia na wote waliokuwa karibu na marehemu, huku akimuomba Mwenyezi Mungu amjaalie Rais Dkt. Samia pamoja na familia yake subira, nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.

Marehemu Hafidh Ameir Hassan anatarajiwa kuzikwa leo Kizimkazi, Zanzibar, katika mazishi yatakayohudhuriwa na familia, ndugu, jamaa, viongozi mbalimbali wa kitaifa pamoja na wananchi.

Rais Dkt. Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu aisamehe roho ya Marehemu Hafidh Ameir Hassan na amjaalie makazi mema Peponi.

Inna Lillahi wa Inna Ilayhi Raji’un.

Leave a Comment