
Dereva wa basi amefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia ajali ya basi la kampuni ya SATCO iliyotokea katika kijiji cha Msembeta, Wilaya ya Dodoma, mkoani Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma iliyotolewa Septemba 8, 2026, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 12:20 asubuhi kwenye barabara ya Singida baada ya basi lenye namba za usajili T 115 EQD lililokuwa likitokea Bukoba kuelekea Dodoma kugongana na lori la kampuni ya Triples lenye namba T 834 EEE na T 161 CUX Semi Trailer aina ya DAF.
Polisi imeeleza kuwa basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Juma Mohamed (40), mkazi wa Dodoma, ambaye alipoteza maisha katika ajali hiyo baada ya gari alilokuwa akiendesha kuligonga lori hilo na kisha kuacha njia kwenda kugonga mti.
Watu watatu walijeruhiwa katika ajali hiyo, ambao ni Sostenes Kusara Sengo, mkazi wa Kahama; Marco Makenzi, mkazi wa Nzega; pamoja na Koplo Korombia Ngonyani, askari wa Polisi wa Kahama.
Majeruhi wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa hospitalini hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi kushindwa kulimudu gari hilo.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuendesha kwa tahadhari na kuheshimu watumiaji wengine wa barabara ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
