
Mshambuliaji wa Tanzania, Clara Luvanga, ametembelea klabu yake ya zamani ya Young Africans (Yanga), ikiwa ni muda mfupi baada ya kukamilisha uhamisho wake wa kihistoria kwenda Washington Spirit ya Marekani.
Luvanga, ambaye alikulia katika mfumo wa Yanga Princess, amerejea katika mazingira ya klabu hiyo wakati akianza ukurasa mpya wa safari yake ya soka katika ligi ya wanawake nchini Marekani.
Septemba 9, 2026, Washington Spirit ilitangaza kumsajili Luvanga kutoka Al-Nassr ya Saudi Arabia kwa mkataba wa miaka minne.

Uhamisho huo umeweka historia kwa Luvanga kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika National Women’s Soccer League (NWSL), ligi ya juu ya soka la wanawake nchini Marekani.
Kabla ya kuhamia Marekani, Luvanga alitumia misimu mitatu akiichezea Al-Nassr, ambapo msimu wa 2025/26 aliweka rekodi ya kuvutia kwa kufunga mabao 24 na kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa ligi.

Ziara yake Yanga imekuja wakati jina lake likizidi kupata umaarufu katika soka la kimataifa, huku hatua yake ya kujiunga na Washington Spirit ikiwa miongoni mwa mafanikio makubwa katika historia ya soka la wanawake Tanzania.
Stori na Anifa Mwegelo | GPL -TUDACO