×

Lamine Yamal Ajiweka Juu ya Mbappe Ballon d’Or 2026

Nyota wa Barcelona, Lamine Yamal, ameongeza presha katika mbio za kuwania tuzo ya Ballon d’Or 2026, akimtaja mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe, kuwa mpinzani wake mkuu katika kinyang’anyiro hicho.

Yamal amesema anaamini yeye na Mbappe ni miongoni mwa wachezaji wawili bora duniani kwa sasa, lakini anaona anastahili zaidi kutwaa tuzo hiyo kutokana na mafanikio aliyoyapata katika msimu uliopita.

Mchezaji huyo wa Barcelona amekuwa na msimu wa kuvutia, akisaidia klabu yake kutwaa ubingwa wa LaLiga, huku akiwa sehemu muhimu ya kikosi cha Hispania kilichotwaa Kombe la Dunia. Aidha, Yamal alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa LaLiga kwa msimu wa 2025/26.

Kwa upande mwingine, Mbappe alikuwa mfungaji bora katika Kombe la Dunia, LaLiga na UEFA Champions League, ingawa hakufanikiwa kutwaa taji kubwa na klabu yake msimu uliopita.

Yamal amesema anajenga hoja yake kutokana na kile alichokifanya uwanjani, akiamini mafanikio ya timu pamoja na mchango wake binafsi vinampa nafasi kubwa ya kutwaa Ballon d’Or mwaka huu.

Mshindi wa Ballon d’Or 2026 anatarajiwa kutangazwa Oktoba 26, 2026, London.

Na Tereza Muga

Leave a Comment