
Dar es Salaam, Tanzania, Alhamisi tarehe 17 Septemba 2026: TOL Gases PLC imefungua Toleo la Hisa za Haki Stahiki lenye thamani ya Shilingi bilioni 8.17 kwa lengo la kugharamia upanuzi wa uwezo wake wa uzalishaji wa hewa ya Carbondioxide, hatua inayoashiria awamu mpya katika mabadiliko ya moja ya kampuni kongwe zaidi za gesi za viwandani na tiba nchini Tanzania.
TOL Gases PLC inatoa hisa mpya za kawaida 11,501,193 kwa bei ya Shilingi 710 kwa kila hisa, kwa wanahisa waliopo wenye sifa, ambapo wanahisa watastahili hisa mpya moja kwa kila hisa tano za kawaida walizokuwa nazo hadi Tarehe ya Kumbukumbu ya Jumatatu, tarehe 14 Septemba 2026.
Toleo hili linafunguliwa tarehe 17 Septemba 2026 na kufungwa tarehe 08 Oktoba 2026 saa 10:00 alasiri. Hisa mpya zitaorodheshwa na kuanza kuuzwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) tarehe 22 Oktoba 2026, kwa kuzingatia masharti husika ya uorodheshaji.
Uchangiaji huu wa mtaji unakuja wakati TOL ikihamia kutoka kipindi cha kujiimarisha kibiashara kuelekea mzunguko mpya wa uwekezaji, ukichochewa na ongezeko la mahitaji ya gesi za viwandani na tiba nchini Tanzania na masoko jirani.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kampuni imerejesha faida, imeimarisha imani ya wateja na kuunganisha uwezo wake wa uzalishaji na usafirishaji. Mapato yameongezeka kwa wastani wa asilimia 9.5 kila mwaka kati ya mwaka 2020 na 2025, huku EBITDA ikiongezeka kwa 28% kati ya mwaka 2024 na 2025. Wakati huo huo, mahitaji yamezidi kujaribu uwezo uliopo wa TOL, huku baadhi ya fursa za kikanda zikizidi uwezo wake wa kusambaza.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TOL Gases, CPA Leonard Kitoka, asema Toleo la Hisa za Haki Stahiki linawakilisha mpito muhimu kutoka hatua ya kujenga upya biashara kuelekea uwekezaji kwa ajili ya awamu yake ijayo.
“Katika miaka mitano iliyopita, tumejenga upya TOL iliyo imara zaidi na yenye uwezo mkubwa wa kuhimili changamoto. Fursa iliyopo mbele yetu sasa ni kubadilisha maendeleo hayo kuwa uwezo wa ziada. Toleo hili la Hisa za Haki linatupatia njia ya kushughulikia pengo la muda mrefu la usambazaji, kuimarisha uaminifu wa huduma na kuiweka kampuni katika nafasi ya kukidhi mahitaji yanayoongezeka nchini Tanzania na kanda nzima.”
Fedha zitakazopatikana zitaelekezwa katika kukuza uwezo wa TOL wa uzalishaji wa hewa ya Carbondioxide (CO2) na miundombinu inayohusiana, ikiwemo usanifu, ununuzi, ufungaji na uanzishaji wa kiwanda kipya cha uzalishaji wa CO2 pamoja na mahitaji ya kiuendeshaji na kilogistiki yanayohusiana.
Uwekezaji huu unashughulikia changamoto halisi inayoikabili kampuni. Mahitaji yameongezeka kwa kasi zaidi kuliko uwezo uliopo wa uzalishaji, jambo linalopunguza uwezo wa TOL kukidhi kikamilifu mahitaji ya ndani na fursa za kikanda.
Mkurugenzi Mtendaji Bw. Daniel Warungu asema uwekezaji huu wa mtaji utaipatia TOL nafasi kubwa zaidi ya kuwahudumia wateja kwa uaminifu, huku ikijenga msingi imara wa uzalishaji kwa ajili ya ukuaji wa baadaye.
“Kimsingi, hii ni hadithi ya uwezo wa uzalishaji. Tumeimarisha biashara, tumeboresha uendeshaji wetu na kurejesha imani ya wateja, lakini sasa mahitaji yanajaribu kikomo cha kile ambacho msingi wetu wa sasa wa uzalishaji unaweza kutoa. Hatua inayofuata ni kuwekeza katika uwezo utakaoiwezesha TOL kuwahudumia wateja wetu kwa uaminifu zaidi na kushindania fursa ambazo kwa sasa hatuwezi kuzihudumia kikamilifu.”
Warungu amesema ukuaji wa TOL utaendelea kwenda sambamba na uwekezaji katika usalama, uendelevu na utawala bora.
“Kwetu, ukuaji lazima uende sambamba na uwajibikaji. Hii inamaanisha kiwango kilekile cha usalama katika kila kituo na kwa kila mteja, mtazamo wa ESG unaojenga thamani ya muda mrefu kwa wadau wetu huku ukichangia vyema katika jamii na mazingira, pamoja na utawala unaoakisi viwango vinavyotarajiwa kwa kampuni iliyoorodheshwa.”
Mradi huu wa CO2 ni sehemu ya mpango mpana wa kukuza uwezo wa uzalishaji.
TOL pia inajiandaa kuanzisha rasmi Kitengo kipya cha Kutenganisha Hewa chenye uwezo wa tani 13 kwa siku, kikiwa kimeungwa mkono na Clinton Health Access Initiative. Ikijumuishwa na kitengo kilichopo cha tani saba kwa siku, uwekezaji huu unatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa oxygen na nitrogen hadi kufikia takribani tani 20 kwa siku ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026.
Uwekezaji huu ukiwa pamoja unalenga kuboresha unyumbufu wa uzalishaji na uaminifu wa usambazaji katika sekta zinazotegemea gesi za viwandani na tiba.
Mpango huu wa upanuzi hauishii kwenye uzalishaji tu. TOL inaongeza magari yake ya usambazaji na kujenga vituo vipya vya usambazaji vya kikanda katika mikoa ya Arusha na Mtwara, sambamba na kituo kilichopo cha Mwanza, ili kusogeza huduma ya uhakika karibu zaidi na wateja nchini Tanzania na kanda nzima.
Jukwaa la uzalishaji la TOL nalo limekua kwa hatua, kutoka EKAMA 1 hadi EKAMA 2, huku EKAMA 3 ikiwa katika hatua za mipango sambamba na kitengo kipya cha kutenganisha hewa, kama sehemu ya ujenzi wa uwezo uliowekwa katika mkakati wa kampuni wa 2025 hadi 2029.
Kwa sasa, TOL inasambaza bidhaa na huduma katika sekta za afya, chakula na vinywaji, uchimbaji madini, uzalishaji viwandani, ujenzi na matumizi mengine ya viwandani. Bidhaa zake ni pamoja na oksijeni, naitrojeni, hewa ya ukaa, asetilini, argoni, heliamu na gesi nyingine za viwandani na tiba, pamoja na mifumo ya gesi za tiba, huduma za kulehemu na kukata vyuma, na vifaa vinavyohusiana.
Historia ya kampuni hii inaanzia mwaka 1950, ilipoanza kufanya kazi Tanzania ikiitwa African Oxygen and Acetylene Company. Ilisajiliwa rasmi mwaka 1966 kama Tanzania Oxygen Limited, kisha ikabadilishwa jina na kuwa TOL Limited mwaka 1996, na baadaye TOL Gases Limited mwaka 2006, kabla ya kubadilika hadhi na kuwa kampuni ya umma iliyoorodheshwa (PLC) kama TOL Gases PLC mwezi Aprili 2024.
Leo hii, TOL inaunganisha uwezo wa uzalishaji, usambazaji na kiufundi ili kuwahudumia wateja nchini Tanzania na masoko ya kikanda, huku usalama, ubora na uhakika wa usambazaji vikiwa nguzo kuu za mfumo wake wa uendeshaji.
Kwa wanahisa, Toleo la Hisa za Haki linatoa fursa kadhaa kulingana na masharti yaliyoainishwa katika Prospectus. Wanahisa wenye sifa wanaweza kuchukua sehemu yote au sehemu ya haki yao, huku wale watakaochukua haki yao yote wakiweza kuomba hisa zisizochukuliwa na wenzao, kulingana na upatikanaji.
Tanzania Securities Limited (TSL) ndiyo Mshauri Mkuu wa Muamala na Wakala wa Udhamini, huku National Bank of Commerce Limited ikiteuliwa kuwa Benki Mpokezi
Wanahisa wenye sifa wanaweza kuthibitisha haki yao kupitia TSL, Programu ya DSE – Hisa Kinganjani, au kupitia Madalali wao wa Hisa. Wanahisa wenye sifa wanashauriwa pia kusoma kwa makini Prospectus ya Toleo la Hisa za Haki kabla ya kufanya maamuzi ya uwekezaji.
Warungu amesema Toleo la Hisa za Haki linapaswa kuangaliwa ndani ya muktadha mpana wa kampuni ya Kitanzania inayojenga uwezo wa uzalishaji unaohitajika kuhudumia uchumi unaokua.
“TOL imekuwa sehemu ya maendeleo ya viwanda nchini Tanzania kwa zaidi ya miongo saba. Jukumu letu sasa ni kuhakikisha kampuni ina uwezo wa uzalishaji, nguvu za kiufundi na ustahimilivu wa kubaki na umuhimu kwa miongo ijayo. Uwekezaji huu unahusu kujenga uwezo huo.”
Toleo la Hisa za Haki Stahiki linafungwa saa 10:00 alasiri, Alhamisi tarehe 8 Oktoba 2026. Wanahisa wanashauriwa kurejea Prospectus kwa masharti kamili, taratibu za maombi, taarifa za malipo na hatari zinazohusika.