×

Kikwete Ahimiza Wanaume Kupima Saratani ya Tezi Dume

 

RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amewataka wanaume kujenga utamaduni wa kupima tezi dume mara kwa mara ili waweze kutibiwa mapema wanapogundulika kuwa na dalili za saratani.

Alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya mwezi wa uelewa wa saratani ya tezi dume yaliyofanyika katika hospitali ya Kairuki Mikocheni.

Rais Kikwete alitembelea mtambo wa kuondoa uvimbe bila upasuaji hospitalini hapo wa High Intensity Focused Ultrasound HIFU ambao unaondoa vimbe mbalimbali mwilini bila upasuaji kwa kutumia mwangwi wa sauti (Ultrasound).

Alisema yeye binafsi ni mwathiriwa wa ugonjwa huo kwani baada ya kugundulika mapema mwaka 2014 alichukua hatua ya kwenda kupima vipimo vingine nchini Marekani na ilipothibitika kuwa na ugonjwa huo alikubali kufanyiwa upasuaji na mpaka sasa ni mzima wa afya.

Aliwataka wanaume wasiogope kwenda kupima saratani ya tezi dume kwani teknolojia kwa sasa imekwenda mbali zaidi na ugonjwa unaweza kuonekana kwa kutumia kipimo cha damu cha PSA tofauti na njia ya zamani ya kutumia kidole.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji wakati ule nilianza kujenga utaratibu wa kupima afya yangu mara nyingi sana na kwa sasa afya yangu ni njema kabisa ndiyo maana mtu akisema naumwa nacheka tu kwasababu afya yangu naijua ni nzuri sana,” alisema

Alisema wakati alipokuwa akipima tezi dume ilionekana kuwa inaongezeka mwaka hadi mwaka lakini madaktari wake walimtia moyo kuwa ni hali ya kawaida na isingeweza kumsababishia madhara kwani inaongezeka taratibu sana.

“Nilikwenda kupima Marekani wakachukua sampuli 14 wakagundua kwenye sampuli mbili kuna dalili ya saratani wakaniambia hakuna wasiwasi wakasema bado kabisa ndiyo inaanza kwa hiyo inatibika bila wasiwasi,” alisema.

“Mimi kwa akili yangu waliposema inatibika nikadhani nitapewa dawa za kumeza kumbe kutibu kwenyewe ni kwa njia ya upasuaji wa kuondoa tezi dume kabisa. Kwasababu tezi dume ikipata saratani hakuna namna nyingine ni kuitoa ili saratani isienee kwingine,” alisema

Aliipongeza hospitali ya Kairuki kwa kuleta mtambo huo wa HIFU ambao unatibu saratani ya tezi dume bila upasuaji na kuondoa vimbe mbalimbali mwilini bila kufanya upasuaji na mgonjwa kuruhusiwa mapema.

“Kwa dhati kabisa nawapongeza kwa kuleta huu mtambo maana namimi nimeuona nimeshangaaa sana nikasema huu mtambo ungekuwepo wakati ule huenda nisingefanyiwa upasuaji wala kuhangaika kwenda Marekani kwa matibabu,” alisema.

Alisema Serikali ikiongeza mitambo kama hiyo ikawa mingi itasaidia kupunguza tatizo la uvimbe kwani watanzania wote hawawezi kutegemea mtambo mmoja pekee uliopo katika hospitali ya Kairuki.

Mtaalamu wa mtambo wa HIFU katika hospitali hiyo, Fredy Felician alisema tangu kusimikwa kwa mtambo huo jumla ya watu 444 wameshahudumiwa kwa kuondolewa vimbe za aina mbalimbali wakati wanaume 95 walitibiwa uvimbe wa saratani ya tezi dume.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Asser Mchomvu alisema takwimu zinaonyesha kuwa saratani ya tezi dume ndiyo inayoongoza kwa wanaume nchini Tanzania na inashika nafasi ya ili kwa saratani za kawaida kwa wanaume duniani.

Alisema saratani ya tezi dume inachangia kati ya asilimia 31.4 na 40 ya kesi zote za saratani zote za wanaume zilizosajiliwa katika vituo vya afya hapa nchini na ni chanzo cha tatu kwa kuongoza kwa vifo vinavyotokana na saratani kwa wanaume nchini ikitanguliwa na saratani ya koo na saratani ya ini.

Aidha, alisema asilimia 43.6 ya wagonjwa hufika hospitalini wakiwa na ugonjwa uliosambaa kwasababu dalili huchelewa kujitokeza na kuongeza kuwa unapogundulika mapema na kuanza matibabu kwa wakati inaweza kutibika.

Leave a Comment