
Mchora katuni maarufu nchini, Kinyagulo Tuzo almaarufu King Kinya, amefariki dunia leo, Septemba 17, 2026 baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rasilimali Watu ya Kampuni ya MCL aliyokuwa akiifanyia kazi kama mchora katuni wa magazeti, imethibitisha taarifa za kifo cha King Kinya.
Kaka wa marehemu, Kiondo Mjema, amenukuliwa akisema King Kinya alianza kuugua akiwa nyumbani Tabata mwanzoni mwa Julai, 2026 hali iliyomfanya kukaa ndani kwa muda kabla ya kupelekwa Morogoro.
Amesema akiwa Morogoro hali yake ilizidi kuwa mbaya na baadaye alipelekwa hospitalini, ambako alilazwa kwa takriban wiki moja kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.
“Alipotoka hospitali aliambiwa arudi tena kwa ajili ya ufuatiliaji. Juzi alirudi hospitalini baada ya kusumbuliwa na tumbo, kuharisha na kutapika, akapewa dawa na kuruhusiwa kurudi nyumbani,” amesema.
Kwa mujibu wa Kiondo, hali ya marehemu ilizidi kuwa mbaya usiku wa kuamkia jana Septemba 15, 2026, akilalamikia maumivu makali ya tumbo na kichwa pamoja na kutapika na kuharisha, ambapo alifariki dunia.
Kiondo amesema msiba upo Kimara Kona na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho Ijumaa Septemba 18, 2026 saa 10 jioni katika makaburi ya Mwananyamala.