×

BRELA Yawataka Wafanyabiashara Kusajili Alama, Kulinda Biashara Zao Afisa Makuka

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wafanyabiashara na wajasiriamali kuhakikisha wanasajili majina na alama za biashara wanazotumia ili kulinda shughuli zao na kuepuka migogoro ya umiliki.

Wito huo umetolewa na Afisa Usajili wa BRELA, Athumani Makuka, wakati wa kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya Tisa ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.

Makuka amesema usajili wa majina ya biashara, kampuni na alama za biashara ni miongoni mwa huduma zinazotolewa na BRELA, huku taasisi hiyo pia ikitoa elimu kuhusu namna ya kulinda ubunifu na uvumbuzi.

“Tunawasistiza wafanyabiashara waje kusajili alama zao kwa sababu kuna kesi ambazo zimejitokeza. Mtu anakuwa na nembo hajaisajili, baadaye mtu mwingine anakuja kuisajili na ndipo mgogoro unaanza,” amesema Makuka.

Aidha BRELA imekuwa ikitoa elimu kwa wabunifu na wavumbuzi kuhusu taratibu za kulinda kazi zao, akieleza kuwa baadhi ya wananchi wamefika katika banda hilo kupata huduma hiyo.

Tumepokea mvumbuzi mmoja kutoka VETA ambaye amekuja kuulizia namna ya kusajili uvumbuzi wake. Hatuwezi kueleza kwa undani uvumbuzi huo kwa sababu bado haujakamilika, lakini tumempa elimu kuhusu hatua zinazohitajika ili uweze kulindwa.

Katika hatua nyingine Makuka amesema BRELA imeboresha mfumo wake wa kidijitali unaojulikana kama BRELA Online System (BOS), kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Hata hivyo mfumo huo umeboreshwa ikilinganishwa na mfumo wa awali, huku ukiwezesha mtumiaji kutumia NIDA moja na akaunti moja katika kupata huduma za BRELA.

Kwa upande wake mhandisi Kutoka Veta Audiface Tarimo amesema amefika katika banda la BRELA baada ya kukumbana na changamoto katika matumizi ya jina la biashara alilolisajili mwaka 2022.

Amesema alihitaji kubadilisha usajili wa jina hilo ili aweze kulisajili kama kampuni, hatua ambayo amepewa msaada na maafisa wa BRELA.

“Nilisajili jina la biashara mwaka 2022, sasa nilihitaji lile jina la biashara kulisajili kama kampuni. Nimefika hapa na nimepata msaada wa kuweza kuhuisha lile jina ili mwisho wa siku niweze kusajili kampuni,” amesema.

Tarimo ameongeza kuwa ameridhishwa na huduma aliyoipata na kuwataka Watanzania wenye changamoto kuhusu huduma za BRELA kufika katika banda hilo ili kupata elimu na msaada.

Leave a Comment