
CHICAGO, MAREKANI: Ulimwengu wa mieleka umeingia kwenye majonzi kufuatia kifo cha ghafla cha mwanamieleka maarufu wa Uingereza, Benjamin Satterley, anayefahamika zaidi ulingoni kwa jina la Pac, akiwa na umri wa miaka 40.
Shirikisho la All Elite Wrestling (AEW) limethibitisha kifo cha Satterley Jumapili Septemba 27, 2026 usiku, taarifa iliyokuja siku moja tu baada ya mwanamieleka huyo kushiriki katika onyesho la “All Out” lililofanyika Jumamosi katika NOW Arena, Hoffman Estates, Illinois, nje kidogo ya Chicago.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi ya Des Plaines, Illinois, iliyotolewa Jumatatu, hakukuwa na dalili za awali za tukio la uhalifu, huku mazingira ya kifo chake yakiwa hayakuonekana kuwa ya kutia shaka. Hata hivyo, chanzo rasmi cha kifo chake hakijawekwa wazi.
Satterley, mzaliwa wa Newcastle upon Tyne, Uingereza, alianza safari yake ya mieleka mwaka 2004 baada ya kuanza mafunzo akiwa na umri wa miaka 18. Alianza kujenga jina katika mashindano ya mieleka ya kujitegemea nchini Uingereza kabla ya kuanza safari ya kimataifa iliyomfikisha katika baadhi ya mashirikisho makubwa zaidi duniani.

Miongoni mwa mashirikisho aliyowahi kucheza ni WWE, AEW, New Japan Pro-Wrestling (NJPW) na Consejo Mundial de Lucha Libre (CMLL).
Safari yake WWE
Satterley alijiunga na WWE mwaka 2012 na akatumia takribani miaka sita katika kampuni hiyo, akitumia jina la Adrian Neville.
Katika kipindi hicho, alifanikiwa kushinda NXT Championship, NXT Tag Team Championship pamoja na WWE Cruiserweight Championship.
Uwezo wake wa kuchanganya nguvu, kasi na mieleka ya kuruka kutoka juu ya kamba ulimfanya apewe jina la utani “The Man That Gravity Forgot”, kutokana na namna alivyokuwa akifanya miondoko ya kuvutia ulingoni.
Jina Pac pia lilikuwa na historia yake binafsi. Satterley aliwahi kueleza kuwa akiwa mtoto alikuwa na misuli ya tumbo iliyokuwa ikionekana kama “six-pack”, jambo lililomfanya baba yake kumpa jina hilo kwa utani. Baadaye jina hilo likawa sehemu ya utambulisho wake wa ulingoni.
Mafanikio ndani ya AEW
Satterley alijiunga na AEW mwaka 2019, ambako baadaye alijulikana kwa jina la “The Bastard”.
Mwaka 2022 alitwaa AEW All-Atlantic Championship, huku pia akiwa sehemu muhimu ya kundi la Death Triangle, pamoja na Penta El Zero Miedo na Rey Fénix, lililofanikiwa kushinda AEW World Trios Championship.
Mwaka 2025, alishinda tena AEW World Trios Championship, safari hii akiwa sehemu ya kundi la Death Riders pamoja na Claudio Castagnoli na Wheeler Yuta.
Ulingoni, Pac alijulikana kwa miondoko yake ya kasi na ustadi mkubwa, ikiwemo shambulio lake maarufu la “Black Arrow” kutoka juu ya kona ya ulingo pamoja na “Brutalizer”, mbinu iliyolenga kumdhibiti mpinzani akiwa chini.
Licha ya taswira yake kali ulingoni, Satterley aliwahi kueleza kuwa nje ya ulingo alikuwa mtu mwenye aibu na aliyekuwa akikabiliana na hofu ya kushindwa na kukataliwa.
Katika mahojiano yake na Colt Cabana kwenye kipindi cha Art of Wrestling, alizungumzia namna alivyokuwa akifanya kazi za zamu za usiku katika kiwanda cha huduma za usafirishaji wakati bado akijaribu kujenga taaluma yake ya mieleka.
Dunia ya mieleka yamkumbuka
Baada ya taarifa za kifo chake kusambaa, jumbe za maombolezo zilianza kutoka kwa wanamieleka mbalimbali.
Mwanamieleka mwenzake wa Uingereza na AEW World Champion, Will Ospreay, alimuelezea Satterley kwa maneno ya heshima, akisema alikuwa mmoja wa watu muhimu kutoka Uingereza na pia binadamu mwenye moyo mkubwa.
Mwanamieleka Evil Uno pia alisema alikuwa katika hali ya mshtuko, akimtaja Satterley kuwa mtu mkubwa, mwenye roho nzuri na mtaalamu wa kweli.
Ace Austin, ambaye alikutana na Satterley ulingoni katika kipindi cha AEW Collision siku chache kabla ya kifo chake, pia alieleza kutokuamini taarifa hizo.
Kifo cha Pac kimeacha pengo katika ulimwengu wa mieleka, hasa kutokana na safari yake ya zaidi ya miaka 20 iliyomfikisha kutoka kwenye mashindano madogo nchini Uingereza hadi kuwa mmoja wa majina yaliyotambulika katika mashirika makubwa ya mieleka duniani.
Stori na Hasina Thabit | GPL