×

Miili ya Chivayo, Mkewe Yatolewa Kwenye Mabaki ya Ndege

Miili ya mfanyabiashara maarufu nchini Zimbabwe, Wicknell Chivayo, mkewe Lucy Muteke na watu wengine watatu waliofariki katika ajali ya ndege, imeondolewa katika eneo la ajali baada ya zoezi la uokoaji na ukusanyaji wa mabaki kuchukua takribani saa 18.

Operesheni hiyo ya kurejesha miili ilikuwa imefanyika leo saa 4:00 asubuhi, huku maafisa wa uchunguzi wa kisayansi wa uhalifu pamoja na wahudumu wa kampuni ya mazishi ya Doves Funeral Services wakikusanya mabaki ya miili katika eneo la ajali.

Mabaki hayo yaliwekwa kwenye mifuko maalumu na kisha kubebwa kwa machela hadi kwenye magari yaliyokuwa yanasubiri eneo hilo.

Eneo la ajali lilikuwa limejaa mabaki ya ndege yaliyoharibika vibaya, huku harufu ya vitu vilivyoungua ikitanda katika eneo hilo. Kwa mujibu wa mashuhuda, hali ilikuwa ngumu kiasi kwamba baadhi ya watu waliofika mapema walipata ugumu kuwatambua wahanga.

Mfanyakazi wa Kudenga Farm, David Yoramu, amesema waokoaji walikumbana na hali mbaya wakati wakijaribu kuzima moto uliokuwa ukiwaka kwenye eneo la ajali.

Amesema walilazimika kutafuta gari maalumu la kubeba maji (water bowser) ili kusaidia kuzima moto kutokana na ukubwa wa tukio hilo.

Baadhi ya ndugu wa Chivayo, akiwemo kaka yake Joachim, walifika eneo la ajali wakati zoezi la ukusanyaji wa mabaki ya miili likiendelea.

Miili hiyo inatarajiwa kufanyiwa taratibu rasmi za utambuzi pamoja na uchunguzi wa kitabibu (post-mortem) kabla ya kukabidhiwa kwa familia kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya Wicknell Chivayo, Lucy Muteke, marubani wawili na mlinzi, baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kuanguka muda mfupi baada ya kuondoka katika makazi yao ya kijijini Gandami.

Leave a Comment