×

Ajali ya Helikopta ya Wicknell Chivayo Mambo Mapya Yafichuliwa

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Zimbabwe (CAAZ) imetoa taarifa za awali kuhusu ajali ya helikopta iliyosababisha kifo cha mfanyabiashara maarufu wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, mke wake Lucy Muteke ‘Lulu’  pamoja na watu wengine waliokuwa ndani ya helikopta hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, helikopta hiyo iliondoka Gandami, Chikomba, eneo ambalo Chivayo na mke wake walikuwa wakijenga nyumba yao ya kijijini.

Helikopta hiyo ilianguka katika eneo la Kudenga Farm, takribani dakika 40 baada ya kuondoka. Ajali hiyo ilitokea Septemba 30, 2026, majira ya saa 11 jioni kwa saa za Zimbabwe.

CAAZ YAFICHUA KILICHOTOKEA ENEO LA AJALI

Mkurugenzi Mkuu wa CAAZ, George Mashababe, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mafuta yalivuja baada ya helikopta kugonga chini, kabla ya moto kuzuka na kuteketeza nyasi katika eneo la ajali.

“Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa mafuta yalivuja wakati wa athari, na kufuatiwa na moto ulioteketeza nyasi katika eneo la ajali,” amesema Mashababe.

Hata hivyo, mamlaka hiyo imesisitiza kuwa bado haijabaini chanzo kilichosababisha helikopta hiyo kuanguka.

MASWALI YAIBUKA MITANDAONI

Taarifa hizo za awali zimeibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya watumiaji wakieleza wasiwasi kuhusu kasi ya kutolewa kwa taarifa za uchunguzi.

Baadhi yao wameibua madai ya uwezekano wa kuwa kuna jambo jingine lililosababisha ajali hiyo, lakini hadi sasa hakuna ushahidi rasmi uliotolewa na mamlaka unaothibitisha madai hayo.

CAAZ bado inaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo ili kubaini chanzo chake na mazingira yote yaliyosababisha helikopta hiyo kuanguka.

Leave a Comment