×

Makamu wa Rais Aitaka Tanesco Kuwezesha Wananchi Kupata Umeme kwa Mkopo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameiagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa kushirikiana na sekta binafsi, kuandaa mpango utakaowawezesha wananchi kununua umeme kwa mkopo wakati wanapokuwa hawana fedha.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi kati ya TANESCO na Benki ya CRDB.

Amesema mpango huo wa ununuzi wa umeme kwa mkopo unaweza kuwa na mfumo unaofanana na huduma za mikopo inayopatikana kwenye mitandao ya simu, ili mwananchi anapohitaji umeme lakini hana fedha aweze kupata huduma hiyo na kulipa baadaye.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, hatua hiyo itasaidia wananchi kuendelea kutumia umeme kwa shughuli za uzalishaji mali pamoja na mahitaji ya majumbani, hasa pale wanapokabiliwa na changamoto za kifedha.

Aidha, ameitaka Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kuendeleza mpango wa kuwaunganisha kwa gharama ya Shilingi 27,000 wananchi wanaoishi katika maeneo yenye mazingira ya kijijini, lakini kutokana na mipaka ya kiutawala wanatambulika kuwa wanaishi mijini.

Amesema kuna maeneo ambayo wananchi wake wanatenganishwa na mipaka ya kiutawala pekee, huku hali zao za maisha zikifanana, hivyo wanapaswa kupata huduma ya umeme kwa gharama inayozingatia mazingira yao ya maisha.

Makamu wa Rais amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kufikia malengo ya kitaifa, ikiwemo Mission 300 na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kwa kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya umeme kwa gharama nafuu.

Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais ameipongeza TANESCO na Benki ya CRDB kwa kuingia katika mpango huo, akisema una lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme na hatimaye kuchangia katika kuboresha maisha ya wananchi.

Leave a Comment