×

Mr. Eazi Aibuka na Kishindo Kipya ‘Comfort’ Akimshirikisha Moliy

STAA wa muziki wa Afropop, Mr. Eazi, amerejea na kazi mpya ya muziki iitwayo “Comfort”, akimshirikisha mwanamuziki kutoka Ghana, Moliy, katika ngoma inayolenga kuwapa mashabiki burudani yenye ladha ya kipekee.

“Comfort” ni wimbo wa kujisikia vizuri unaochanganya sauti ya kipekee ya Mr. Eazi inayotambulika kupitia mtindo wake wa Banku Music na sauti laini ya Moliy, anayefahamika pia kupitia wimbo wake “Shake It To The Max.”

Wimbo huo umebeba mchanganyiko wa Afrobeats, Dancehall na R&B, ukiwa na midundo ya kustarehesha na melodi inayoshika, huku wasanii hao wakitumia mitindo yao kuleta hisia za furaha na mahaba.

Uzalishaji wa “Comfort” umefanywa na mtayarishaji wa Nigeria, Ragee, anayehusishwa na baadhi ya kazi zilizopata umaarufu hivi karibuni, zikiwemo “Unavailable” ya Davido pamoja na “Hot Body” na “Who’s Dat Girl” za Ayra Starr.

Akizungumzia wimbo huo, Mr. Eazi amesema “Comfort” ni mwendelezo wa sauti yake, lakini ukiwa na mtazamo wa muziki mwepesi na wa kuwapa wanawake heshima.

“Hii ni toleo lililoboreshwa la sauti yangu ya kipekee. Ninatengeneza muziki wa kina dada, muziki mtamu, mwepesi, unaowasifia kina dada. Ni kuhusu kuweka mambo mepesi, ya kufurahisha na yanayokufanya ujisikie vizuri,” amesema.

Ameongeza kuwa pamoja na kujaribu ladha hiyo mpya, bado amehakikisha mashabiki wanapata sauti wanayoifahamu kutoka kwake.

“Comfort” imekuja katika kipindi ambacho Mr. Eazi ameendelea kushirikiana na wasanii na watayarishaji kutoka maeneo mbalimbali katika kuendeleza muziki wake.

Mapema mwaka 2026, Mr. Eazi alishirikiana na mtayarishaji wa Dancehall kutoka Marekani, Dre Skull, katika mfululizo wa nyimbo zilizojumuisha “Lambo” akiwa na Vybz Kartel, “Hide Your Love” na “Remember That” akiwa na gwiji wa Dancehall, Cham.

Kupitia “Comfort”, Mr. Eazi na Moliy wameendelea kuunganisha ladha za Afrobeats, Dancehall na R&B, wakilenga kuleta sauti nyepesi na ya kuburudisha kwa mashabiki wa muziki.

NA MWANDISHI WETU

Leave a Comment