
LIWALE, LINDI — Wajawazito wanaohudumiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi wanatarajiwa kunufaika na vifaa mbalimbali vya uchunguzi na kujifungulia vilivyotolewa na Kampuni ya Mawasiliano ya Yas Tanzania kupitia Kampeni ya ‘Tumaini’.
Msaada huo unajumuisha kitanda cha uchunguzi kwa wajawazito, kiti mwendo, mashuka, trei za kujifungulia (delivery trays) pamoja na khanga. Vifaa hivyo vinatarajiwa kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma bora kwa akina mama wajawazito, hususan wakati wa kujifungua.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Dkt. Hadija Said Kitiku, alisema vifaa vya uzazi ni miongoni mwa mahitaji muhimu katika hospitali hiyo na kwamba msaada huo utawasaidia wahudumu wa afya kuboresha huduma kwa wajawazito.

Alisema uwepo wa vifaa vya kutosha unawapa madaktari na wauguzi mazingira bora ya kufanya uchunguzi na kuwahudumia akina mama kwa ufanisi wakati wa kujifungua.
“Tunapokuwa na vifaa vya kutosha, madaktari na wauguzi wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufanya uchunguzi na kuwahudumia kwa ufanisi akina mama wakati wa kujifungua,” alisema Dkt. Kitiku.
Aliongeza kuwa kitanda cha uchunguzi, kiti mwendo na trei za kujifungulia vilivyotolewa ni miongoni mwa vifaa vinavyohitajika katika utoaji wa huduma za kila siku hospitalini hapo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Yas Kanda ya Pwani Kusini, Erick Munaku, alisema Kampeni ya Tumaini ilianzishwa baada ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kuguswa na changamoto zinazowakabili baadhi ya akina mama wakati wa ujauzito na kujifungua.
Alisema wafanyakazi hao waliamua kushirikiana na taasisi za afya kwa kuchangia vifaa vinavyolenga kuboresha mazingira ya huduma kwa mama na mtoto.
“Tumaini ilianza na sisi wafanyakazi kujiuliza tunaweza kufanya nini kusaidia mama anayekwenda kujifungua. Tukaona ni vyema kuchangia vifaa vinavyomgusa mama mjamzito kwa kutambua changamoto mbalimbali ambazo wanakutana nazo hususan wakati wa kujifungua,” alisema Munaku.
Munaku alisema Yas kupitia kampeni hiyo imekuwa ikishirikiana na taasisi za afya katika maeneo mbalimbali nchini kubaini mahitaji na kuchangia vifaa vinavyoweza kusaidia kuboresha huduma za uzazi.
Aliwashukuru madaktari, wauguzi na watoa huduma wengine wa Hospitali ya Wilaya ya Liwale kwa kazi wanayoifanya ya kuwahudumia akina mama na watoto, akisisitiza kuwa msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi zao.
Msaada huo unatarajiwa kuchangia kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya ya uzazi katika Hospitali ya Wilaya ya Liwale, huku ukilenga kumsaidia mama na mtoto katika kipindi muhimu cha ujauzito na kujifungua.