
HARARE, ZIMBABWE: Mfanyabiashara maarufu na mwenye utata nchini Zimbabwe, Wicknell Chivayo, amezikwa katika Makaburi ya Glen Forest siku ya Alhamisi Oktoba 8, 2026 katika mazishi yaliyotawaliwa na magari ya kifahari, watu mashuhuri na shamrashamra zilizoakisi maisha ya anasa aliyokuwa akiishi.
Msemo wa Kiingereza “Even the mightiest oak falls at last”, unaomaanisha kuwa hata mti mkubwa na wenye nguvu hatimaye huanguka, umeelezwa kuwa unaakisi mwisho wa maisha ya Chivayo, ambaye alijizolea umaarufu kutokana na utajiri wake, ukarimu uliotangazwa hadharani na maisha ya kifahari.

Katika kipindi cha uhai wake, Chivayo alijulikana kwa kutumia fedha nyingi kununua magari ya kifahari kwa ajili yake mwenyewe na watu mashuhuri, akieleza vitendo hivyo kama sehemu ya shughuli zake za kusaidia wengine.

Hata hivyo, maisha yake yaligawanya maoni ya wananchi. Wapo waliomwona kama mfanyabiashara mkarimu aliyependa kuwainua wengine, huku wengine wakihoji chanzo cha utajiri wake na kuona maisha yake ya kujionyesha kwa anasa kuwa yalipindukia.
Hata kifo chake kimeendelea kuibua mijadala, hasa kuhusu mazingira ya ajali ya helikopta iliyosababisha vifo vyake na mkewe, Lucy Muteke, katika eneo la Marondera wiki iliyopita, kwa mujibu wa taarifa ya awali.

Magari ya kifahari yatamalaki mazishi
Msafara wa magari ya kifahari ulipita katika Barabara ya Domboshava, ambayo ina mashimo, kabla ya kuingia katika mitaa yenye vumbi ya Hatcliff, ambako waombolezaji walikusanyika kushuhudia msafara wa mazishi.
Kwa baadhi ya watu waliokuwa kando ya barabara, kupata nafasi ya kuuona jeneza la Chivayo lililofunikwa kwa bendera ya Zimbabwe kulikuwa jambo muhimu katika siku hiyo ya kuaga.

Watu mashuhuri waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na wanamuziki Jah Prayzah na Seh Calaz, mhubiri Uebert Angel, Pokello Nare, Mudiwa Good na Nathan Mutasa, pamoja na waumini wa madhehebu ya kitume.

Katika eneo la Makaburi ya Glen Forest, rangi nyeusi na nyeupe zilitawala shughuli za mazishi, katika hafla iliyodhihirisha umaarufu na hadhi aliyokuwa nayo Chivayo alipokuwa hai.
Serikali yatambua mchango wake
Akitoa salamu za rambirambi, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Masuala ya Mikoa, Charles Tavengwa, amesema kifo cha Chivayo ni pigo kwa jumuiya ya wafanyabiashara na taifa la Zimbabwe kwa ujumla.
Tavengwa amesema Chivayo alikuwa mfanyabiashara mashuhuri ambaye shughuli zake zilienea katika maeneo mbalimbali ya Zimbabwe na nchi jirani.

Amesisitiza kuwa kutambuliwa kwa mchango wake katika jamii na shughuli zake za hisani kunaleta wajibu wa kuenzi kumbukumbu yake kwa heshima na utu.
Kwa mujibu wa waziri huyo, Zimbabwe inahitaji wafanyabiashara, uwekezaji na uzalishaji ili kuendeleza uchumi wake, hivyo kifo cha Chivayo ni pigo katika kipindi ambacho taifa linahitaji mchango wa sekta binafsi.

Mwisho wa maisha yaliyojaa utata na anasa
Mazishi ya Chivayo yamehitimisha maisha ya mtu aliyekuwa akivutia hisia tofauti katika jamii ya Zimbabwe, kutokana na utajiri wake mkubwa, ukarimu aliouonyesha hadharani na maswali yaliyokuwa yakizunguka maisha yake ya kifedha.
Mwili wake na wa mkewe, Lucy Muteke, vilishushwa makaburini katika tukio lililofunga ukurasa wa maisha yao yaliyokatizwa na ajali ya helikopta.
Hata hivyo, licha ya mazishi hayo ya kifahari na heshima aliyopewa na baadhi ya viongozi na watu mashuhuri, mijadala kuhusu maisha yake na mazingira ya kifo chake inaendelea kuacha maswali katika jamii ya Zimbabwe.