
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Cuthbert Sendiga, na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Mongoso Wambura, kufuatia vifo vya watu 32, wakiwemo askari polisi watatu, vilivyotokana na ajali mbili tofauti za barabarani zilizotokea usiku wa kuamkia Oktoba 9, 2026, mkoani Morogoro.
Katika salamu hizo, Rais Samia ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, ndugu, jamaa na marafiki, huku akiwaombea nguvu, subira na faraja katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Aidha, amewatakia majeruhi wote wa ajali hizo kupona haraka na kurejea katika hali zao za kawaida.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amelielekeza Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia sheria za usalama barabarani, huku akiwahimiza madereva na watumiaji wengine wa barabara kuchukua tahadhari na kuzingatia sheria ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.
Rais amehitimisha salamu zake kwa kumuomba Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu mahali pema peponi.
Salamu hizo zimetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Shaaban Kissu, jijini Dar es Salaam, Oktoba 9, 2026.
