
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kuwa itatumia vifaa maalumu vya kupima ubora wa hewa (Gas Detectors) kukagua vyumba vya kubadilishia nguo vya Simba na Yanga katika mchezo wa Derby ya Kariakoo leo Oktoba 10, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB iliyotolewa Oktoba 9, 2026, ukaguzi huo utafanyika baada ya vyumba hivyo kukabidhiwa kwa timu husika na utaendelea hadi mchezo utakapokamilika.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha usalama wa wachezaji, benchi la ufundi na maafisa wa timu, pamoja na kudhibiti uwepo wa gesi au hewa isiyo salama ambayo inaweza kuhatarisha afya zao.
TPLB imeeleza kuwa matumizi ya vifaa hivyo yalianza Oktoba 8, 2026, na utaratibu huo unahusu viwanja vyote nchini vinavyotumika kwa michezo ya ligi.
Aidha, bodi hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mechi za Ligi Kuu Tanzania zinafanyika katika mazingira salama, kwa kuzingatia taratibu na viwango vya usalama vinavyotakiwa.
