×

Watatu Wafariki Baada ya Pikipiki Kugongana na Lori Korogwe

TANGA: Watu watatu wamefariki dunia katika ajali ya barabarani iliyohusisha gari la mizigo aina ya HOWO na pikipiki aina ya SINORAY katika eneo la Goha, Mombo, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga leo, Oktoba 16, 2026, imeeleza kuwa ajali hiyo imetokea majira ya saa 10:10 alfajiri katika barabara ya Same–Korogwe.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gari hilo lenye namba za usajili T.257 ESA, lililokuwa na tela lenye namba T.263 ESA, lilikuwa likitokea Moshi kuelekea Korogwe lilipogongana uso kwa uso na pikipiki hiyo iliyokuwa imebebeba abiria watatu.

Ajali hiyo imesababisha vifo vya watu watatu, wakiwemo dereva wa pikipiki na abiria wake wawili. Miili ya marehemu imehifadhiwa huku uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha ajali hiyo ukiendelea.

Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa pikipiki kupita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari katika eneo ambalo haliruhusiwi kufanya hivyo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, ikiwemo kuepuka kuyapita magari mengine katika maeneo yenye alama zinazokataza kitendo hicho.

Aidha, Jeshi hilo limewataka watumiaji wa barabara kuzingatia mwendo kasi unaoruhusiwa na kuchukua tahadhari wakati wote ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo na majeraha.

Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi limeendelea kuhimiza uwajibikaji na utii wa sheria za usalama barabarani kwa lengo la kulinda maisha ya watumiaji wote wa barabara.

Leave a Comment