
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamsaka mwanamke ambaye bado hajafahamika, anayetuhumiwa kumtelekeza mtoto mchanga wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa siku tatu katika eneo la Mieresini B, Kata ya Makuyuni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Oktoba 12, 2026, tukio hilo limetokea Oktoba 12, 2026, majira ya saa 3:30 asubuhi, ambapo mtoto huyo alikutwa akiwa hai baada ya kutelekezwa kwenye kibaraza cha nyumba isiyotumika katika eneo hilo.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi kubaini mazingira ya tukio hilo pamoja na kumtafuta mwanamke anayedaiwa kumtelekeza mtoto huyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Aidha, mtoto huyo amekabidhiwa kwa Maafisa wa Ustawi wa Jamii katika Kituo cha Himo kwa ajili ya taratibu za malezi na uangalizi zaidi.
