
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya udhibiti na usimamizi wa Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) ili kulinda fedha za wanachama, kuongeza uwazi na uwajibikaji pamoja na kuhakikisha taasisi hizo zinaendana na mabadiliko ya teknolojia na masoko ya kifedha.
Dkt. Mwigulu alitoa msisitizo huo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika Kongamano la Kimataifa la Vyama vya Akiba na Mikopo Barani Afrika, SACCA Congress 2026, akieleza kuwa mifumo imara ya usimamizi ni muhimu katika kuimarisha uaminifu wa wanachama na kuhakikisha vyama hivyo vinaendelea kutoa huduma bora za kifedha.
Alisema Tanzania inaendelea kuboresha mfumo wa usimamizi wa SACCOS kwa kuunganisha misingi ya ushirika na viwango vya tahadhari za kifedha ili kuhakikisha taasisi hizo zinaendeshwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu zinazolinda maslahi ya wanachama.
Alifafanua kuwa mfumo huo unalenga kuhakikisha SACCOS zinazingatia masuala ya mtaji, ubora wa mali, mapato na usimamizi bora wa fedha, huku zikidumisha uwazi na uwajibikaji katika shughuli zake.
Aidha, alihimiza nchi za Afrika kuimarisha mifumo ya usimamizi na kuweka mikakati ya kukuza taasisi za ushirika katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili ziweze kukabiliana na changamoto za sekta ya fedha na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alizitaka taasisi za kifedha za ushirika, hususan SACCOS, kubuni huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya sekta za uzalishaji, ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na biashara.
Alisema huduma hizo zinapaswa kuwawezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji, kuongeza ajira na kipato pamoja na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi.
Chongolo alieleza kuwa upatikanaji wa huduma za kifedha zenye gharama nafuu na zinazokidhi mahitaji ya wakulima ni muhimu katika kuwawezesha kuwekeza kwenye pembejeo, teknolojia za kisasa, mitambo ya kilimo, uchakataji wa mazao na upatikanaji wa masoko.
Alisisitiza kuwa SACCOS zinapaswa kuhakikisha fedha zinazokusanywa kutoka kwa wanachama zinaelekezwa zaidi