
MKONGWE wa Muziki wa R&B na Afro-Pop, Judith Wambura ‘Jide’ usiku wa kuamkia Jumapili aligawa tuzo kwa marafiki zake wa karibu waliochangia katika maisha na muziki wake.
Tukio hilo lilijiri katika Ukumbi wa Sky Night Life uliopo Masaki jijini Dar ambapo Jide alikuwa akizindua wimbo wake mpya wa Ndi Ndi Ndi.
Katika tuzo hizo, Jide alimpa DJ Choka kama mtu muhimu katika muziki wake huku tuzo nyingine ya heshima ikienda kwa Mbunge wa Viti Maalum CCM Arusha, Catherine Magige, mbunifu wa mavazi, Khadija Mwanamboka naye alipata, Rama Dee naye alipata tuzo kama msanii mwenzake mwenye mchango mkubwa kwake na wengine wengi.
Mbali na utoaji wa tuzo hizo sambamba na uzinduzi, Jide alisema kuwa amerudi upya kimuziki na kuongeza kuwa sanaa ni ubunifu na kwamba ukifanya kitu kilekile watu wanakuchoka kwa hiyo ni lazima awe anabadilika ili asizoeleke.