×

Dkt. Mwigulu Aongoza Mjadala Wa Uwekezaji Kwenye Kilimo Biashara

WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya kilimo biashara nchini, akieleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi zinazoweza kuchochea uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kupanua masoko.

Dkt. Mwigulu amesema uwekezaji nchini Tanzania unaweza kuwafikia watumiaji katika soko la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati lenye watu takribani milioni 170, hivyo kutoa fursa kwa wawekezaji kupanua shughuli zao za kibiashara.

“Uwekezaji unaweza kuchangia kutoa huduma za chakula na lishe na wakati huohuo ukatengeneza fursa za kiuchumi zinazoonekana. Kwa hiyo, tunawakaribisha nyote kuwekeza nchini Tanzania kwani mnapowekeza Tanzania, kwa maana pana, mnawekeza pia katika soko la ukanda mzima,” amesema.

Akizungumzia maeneo yenye fursa za uwekezaji, Waziri Mkuu ametaja usindikaji na ufungashaji wa mazao, ujenzi wa maghala, miundombinu ya kuhifadhi bidhaa katika ubaridi, usafirishaji, huduma za kidijitali pamoja na huduma za kifedha kwa wakulima na wafanyabiashara.

Dkt. Mwigulu ameyasema hayo Jumanne, Oktoba 20, 2026, wakati akiongoza mjadala kuhusu uwekezaji katika kilimo biashara uliohusisha viongozi wa kampuni zinazojihusisha na utafiti wa kilimo, teknolojia za kilimo, uzalishaji wa bidhaa za kilimo, mbegu na dawa za kuzuia wadudu waharibifu wa mazao.

Mjadala huo umefanyika kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), jijini Des Moines, katika Jimbo la Iowa, Marekani.

Akifafanua kuhusu uwezo wa Tanzania katika uzalishaji wa kilimo, Dkt. Mwigulu amesema nchi ina hekta milioni 44 za ardhi inayofaa kwa kilimo, lakini ni hekta milioni 10.8 pekee zinazotumika kwa shughuli hizo.

Kuhusu kilimo cha umwagiliaji, amesema Tanzania ina uwezo wa kumwagilia hekta milioni 29.4, huku eneo linalotumika kwa sasa likiwa dogo ikilinganishwa na uwezo huo. Hali hiyo, kwa mujibu wa maelezo yake, inaonesha uwepo wa fursa za uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji na uzalishaji wa mazao.

Aidha, amesema Serikali imewekeza katika skimu za umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu na programu zinazolenga kuwawezesha vijana kushiriki katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Ameongeza kuwa Serikali pia imeweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuvutia mitaji na kukuza shughuli za kiuchumi nchini.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko, kutengeneza ajira zenye staha na kuimarisha usalama wa chakula na lishe nchini.

Boresha kichwa kiwe cha habari zaidiFupisha habari kwa matumizi ya mtandaoni

Leave a Comment