
Iran imesema haitakuwa tayari kufanya mazungumzo na Marekani hadi matakwa yake yatimizwe, hatua inayoashiria msimamo mkali wa Tehran licha ya juhudi za upatanishi zinazofanywa na Pakistan.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Iran zilizoripotiwa na Reuters, ujumbe huo uliwasilishwa Jumanne, Oktoba 20, 2026, wakati Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, alipokutana na Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Field Marshal Asim Munir, mjini Tehran, kujadili juhudi za upatanishi na hali ya usalama katika eneo hilo.
Pakistan imekuwa mpatanishi muhimu kati ya Marekani na Iran. Juhudi za awali za nchi hiyo zilisaidia kufikiwa kwa makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano mwezi Juni, lakini makubaliano hayo yalivunjika baada ya mapigano kati ya mataifa hayo kuanza tena wiki chache baadaye.
Katika mazungumzo tofauti na Munir, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, alisema Marekani haiwezi kurejesha imani ya Tehran hadi itimize masharti saba yaliyowekwa na Iran mwezi uliopita kwa ajili ya kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz.
Masharti hayo yanajumuisha kusitishwa kwa zuio la Marekani dhidi ya bandari za Iran, kuondolewa kwa vikwazo vinavyoathiri mauzo ya mafuta ya Iran na kukomeshwa kwa uhasama katika maeneo yote ya mapigano ya kikanda.
Mkuu wa masuala ya usalama wa Iran, Mohsen Rezaei, alitoa ujumbe kama huo katika mkutano mwingine na Munir, akisisitiza kuwa Tehran haitafanya mazungumzo na Washington hadi matakwa yake yatimizwe.
Rezaei pia alisema Iran itahifadhi ndani ya nchi yake nyenzo zote za nyuklia zilizorutubishwa, akisisitiza msimamo wa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Mojtaba Khamenei, kwamba urani iliyorutubishwa kwa kiwango kinachokaribia kutumika kutengeneza silaha za nyuklia haitapelekwa nje ya nchi.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, alisema mapema mwezi huu kuwa Iran inapaswa kupunguza kwa kiwango kikubwa uwezo wake wa kurutubisha urani ili kukidhi matakwa ya Washington na kumaliza vita vinavyoendelea kati ya mataifa hayo kwa takribani miezi minane.
Marekani, Israel na mataifa mengine ya Magharibi yamekuwa yakiishutumu Iran kwa kutafuta silaha za nyuklia. Wasiwasi huo umeongezeka kutokana na hatua ya Iran kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 60, ambacho ni cha juu kuliko kinachohitajika kwa matumizi mengi ya kiraia na kinakaribia kiwango cha asilimia 90 kinachohusishwa na urani inayotumika kutengeneza silaha za nyuklia.