NAMSHUKURU sana Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo Jumanne nyingine. Ni neema yake ndiyo imeweza kunifikisha hapa, kwani kuna wengi walitamani kufika lakini wameshindwa.
Mada yangu ya leo inahusu wapendanao na maisha yao ya kila siku. Wengi wanashindwa kujua kwamba, kati ya mambo yanayoharibu upendo kwa wapendanao ni msongo. Lakini naomba nifafanue kwa kusema msongo wa mawazo au stress kwa Kimombo.
Msongo wa mawazo ni sumu kubwa sana kwa wanandoa na wale wasio katika ndoa, lakini wanaishi kwa matumani kuwa tayari wamekuwa wamoja.
UGOMVI
Wapo wanandoa ambao kugombana kwako ni kama jadi. Katika siku saba za wiki, hutokea wakawa salama siku moja mpaka mbili, zilizobaki ni kugombana kwa kwenda mbele.
Hali hii huwafanya wengi kuamini wanashindwa kuishi pamoja au kuchokana. Wengine wanaochokana ni wale wanaoishi maisha ya ugomvi wa mara kwa mara.
MATUMIZI YA MANENO
Tena kuna wanandoa wengine wanapogombana wanatumia maneno makali ambayo yanapotwama kwenye akili ya aliyeambiwa, kutoka huchukua muda mrefu au yasitoke kabisa na ndiyo chanzo cha msongo kwani humfanya mwenzako kila wakati awaze hayo na kupoteza ladha ya upendo.
SIKIA MFANO HUU
Mfano mzuri, wanandoa wanapogombana kwa kutupiana maneno mabaya, inafika mahali mmoja anamwambia mwenzake; ‘kwanza wewe najuta, sijui kwa nini niliamua kuwa na wewe’. Au; ‘wewe hufai kabisa, siku ukifa nitafurahi sana, nitakuwa huru’. Au; ‘nilikukuta huna kitu wewe, sasa umepata unajifanya kuninyanyasa.’
Maneno yenye mfano huo kusema kweli yanaharibu sana upendo. Kama mwenzako alizoea akirudi nyumbani amekubebea ‘vijizawadi’ utaanza kuona havipo. Na si ajabu wewe uliyekuwa ukibebewa zawadi, ukaja juu tena na kuuliza; ‘kwa nini zawadi haziji siku hizi au kuna sehemu unazipeleka nini?’
Lakini kumbe umesahau kwamba, matumizi ya maneno yako kwenye ugomvi ni mabaya sana na ndiyo yamemfanya mwenzako ‘atumbukiwe nyongo’ na wewe.