ILIPOISHIA
Sikutaka kubaki humo, nilichokifanya ni kuinuka, kuvaa nguo zangu na kutoka ndani ya mochwari ile. Walinzi walikuwa wakipiga stori, sikujali, nikatoka mpaka nje, nilipofika huko, nikamkuta mganga akiwa na tabasamu pana kabisa huku akitingisha kichwa chake juu chini, chini juu kuonesha kukubaliana na kile kilichofanyika.
SONGA NAYO
Mganga alinipa uhakika kwamba kila kitu kingekuwa kama kilivyotakiwa kuwa. Kwa kweli nilimwamini sana na kuona kuwa hivi karibuni ningekuwa tajiri mkubwa mno nchini Tanzania na hivyo kurudi kijijini nikiwa shujaa.
Siku iliyofuata, mganga akaniambia nirudi nilipokuwa nikiishi ambapo sikutakiwa kumwambia mtu yeyote juu ya kile kilichokuwa kimetokea. Sasa ratiba ikawa ni kwenda kwa mganga kila siku, ananichukua kimazingara na kunipeleka mochwari ambapo kama kawaida nilikuwa nikiendelea kufanya mapenzi na maiti.
Siku ya kwanza niliogopa sana lakini siku zilivyokwenda, hofu ikaniondoka na hivyo kuwa na ushujaa mkubwa moyoni mwangu. Nilipitia mengi kipindi hicho, wakati mwingine nililetewa maiti zilizoungua moto, zilitisha sana lakini ilikuwa ni lazima nifanye nazo mapenzi, wakati mwingine nililetewa maiti zilizopata majanga mengine, zote hizo, nilivumilia.
Siku zilikatika mpaka nilipobakiza maiti moja. Mganga akaniambia kwamba hiyo sikutakiwa kufanya nayo kule mochwari bali nilitakiwa kufanya nayo sehemu nyingine kabisa, tena makaburini.
Kwa kweli niliogopa sana, sikujua kitu kilichonitisha kwani kiukweli kati ya makaburini na mochwari, mochwari kulitisha zaidi. Usiku, mganga akanichukua na kunipeleka katika makaburi fulani yaliyokuwa jijini Dar. Nilipofika karibu na makaburi hayo, akaniambia niingie ndani ya eneo la makaburi kisha kuelekea katika kaburi la jamaa mmoja aliyekufa miaka kumi iliyopita, huyo jamaa aliitwa Samweli Ramadhani.
“Nitalijuaje?”
“Utalijua tu, una uwezo mkubwa wa kulijua kaburi hilo, wewe nenda,” aliniambia mganga.
Wakati nimeingia ndani ya eneo la kaburi hilo, kwa macho yangu niliweza kuwaona wachawi, walikuwa zaidi ya ishirini, walisimama pembeni ya kaburi moja la mtoto ambapo maiti yake ilikuwa ikihitajika sana.
Sikujua kwa nini, sikufika pale kuwafuatilia wachawi wale niliowaona ila wao hawakuniona, nilifika pale nikiwa na mambo yangu, hivyo sikujali. Nilitembea kwa tahadhari, makaburini kulitisha sana, kulisisimua sana.
Nilipofika katika kaburi moja, nikasimama, sikujua kama lilikuwa lenyewe au jingine, nikasogelea kuangalia jina, nikakuta limeandikwa Samweli Ramadhani, nikashangaa, nimejuaje kama hilo kaburi ndilo lenyewe.
“Ila kwa nini maiti hii?” nilijiuliza, ghafla nikasikia mganga akinijibu.
“Kwa imani zetu wanadamu, tunasema jina la Samweli ni la Kikristo na Ramadhani ni la Kiislamu, hivyo ukifanya mapenzi na maiti hii, Wakristo na Waislamu wote watakuheshimu na utajiri wako utamsisimua kila mtu,” nilimsikia vema mganga huyo.
Nilisimama huku nikiwa sijui nini cha kufanya, nilisubiri maelekezo, nikaisikia sauti ya mganga ikiniambia nisubiri, nikafanya hivyo, ghafla, katika hali ambayo sikuitarajia, nikaona hirizi kubwa ikiwa imefungwa kiunoni mwangu, ilikuwa nzito, kilichonishangaza, hirizi ile kama ilikuwa na moyo, kwani niliweza kuyasikia mapigo kama ya moyo yakidunda kutoka katika hirizi hiyo.
Ghafla, upepo mkali ukaanza kuvuma mahali hapo, matawi ya miti iliyokuwa makaburini yakaanza kuyumbishwa huku na kule. Nikasikia kelele za watu wengi, sikujua zilitoka wapi lakini nilizisikia masikioni mwangu.
Nikaanza kutetemeka, mara nikahisi kama kuna mtu alikuwa nyuma yangu, sikugeuka kujua alikuwa nani, mtu huyo akanisogelea na kunishika bega kwa nyuma, pumzi zake nilisikia vema karibu kabisa na masikio yangu. Nikashindwa kuvumilia, nikageuka, cha kushangaza sikumuona mtu.
Wakati nikiendelea kutetemeka kaburini pale, ghafla nikaliona lile kaburi likianza kujifukua lenyewe ndani yake kulikuwa na jeneza likiwa limefunguliwa lakini halikuwa na maiti, nikashangaa sana.
Ghafla mwili wangu ukaanza kusisimka, nikahisi tena nyuma yangu kulikuwa na mtu, nilitaka kugeuka, nikashindwa kufanya hivyo, nikahisi nikishikwa bega kwa nyuma, nilitetemeka zaidi, kijasho chembamba kikanitoka mno.
“Unanukia vizuri mpenzi wangu!” nilisikia sauti hiyo nyuma yangu, nikazidi kutetemeka.
“Wewe nani?” nilijikuta nikiuliza huku mihemo ya mtu huyo ikisikika vema nyuma yangu.
Itaendelea wiki ijayo.