
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi za taasisi mbalimbali nchini, zikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 23, 2026, na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jenerali Mstaafu George Marwa Waitara ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Katika uteuzi mwingine, Rais Samia amemteua Bi. Zuhura Sinare Muro kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), taasisi inayohusika na masuala ya utalii nchini.
Aidha, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Rajab Semfuko ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
