×

Tpsf Yaimarisha Mitandao Ya Biashara na Kufungua Fursa za Uwekezaji Kanda ya Ziwa

Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limefanikiwa kuandaa tukio la kimkakati la mitandao ya biashara jijini Mwanza, lenye kaulimbiu “Kuunganisha Biashara, Kufungua Fursa” (Connecting Businesses, Unlocking Opportunities), kwa lengo la kuimarisha mahusiano ya kibiashara, kukuza ushirikiano na kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji katika Kanda ya Ziwa.

Tukio hilo limewakutanisha viongozi wa serikali, wadau wa biashara, wajasiriamali na wawakilishi wa sekta binafsi kutoka maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa, likiwa jukwaa la kujadili fursa za kibiashara, kuimarisha ushirikiano na kukuza maendeleo ya sekta binafsi.

Mgeni Rasmi katika tukio hilo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa CP Salum Hamiduni, ambaye aliungana na Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mheshimiwa William Kafiti, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw. Ephraim Mafuru. Pia, tukio hilo lilihudhuriwa na wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali.

Kupitia jukwaa hilo, umuhimu wa mitandao ya kimkakati ya biashara, ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, pamoja na kujenga mahusiano yenye tija, umeendelea kusisitizwa kama nyenzo muhimu katika kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na kuchochea maendeleo endelevu ya uchumi.

Tukio hilo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania kwa kuwezesha wafanyabiashara na wajasiriamali kuunganishwa na wadau muhimu, kutambua fursa zilizopo na kujenga ushirikiano unaoweza kuleta matokeo chanya katika ukuaji wa biashara na uwekezaji.

Leave a Comment