
Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, anatarajiwa kufika mahakamani Januari 10 kwa ajili ya kusikiliza hukumu yake, zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kuapishwa kwa muhula wake wa pili kama Rais wa Marekani.
Jaji Juan Merchan, kupitia uamuzi wa kurasa 18 uliotolewa Ijumaa, aliamuru Trump kufika mahakamani kwa njia ya mtandao au binafsi ili kupokea hukumu yake. Uamuzi huo pia ulikataa ombi la Trump la kutupilia mbali hatia aliyopewa kwa makosa 34 ya kubadilisha kumbukumbu za biashara, makosa yanayohusiana na malipo ya kificho yaliyotolewa wakati wa kampeni zake za urais mwaka 2016.
Trump alikuwa ametoa hoja ya kufuta mashtaka hayo kufuatia ushindi wake kwenye uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba. Hata hivyo, hukumu hiyo imepangwa kufanyika siku 10 kabla ya hafla ya kuapishwa kwake inayotarajiwa kufanyika Januari 20.