
Dar es Salaam, Tanzania, Jumatano, tarehe 28 Oktoba 2026 – Tanzania Breweries Plc (TBL) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya kuanzisha Mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Ujuzi-Kwanza. Ushirikiano huu unalenga kukuza ujuzi wa vitendo katika kilimo, kuunda fursa kwa vijana na kuchangia mabadiliko ya sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Mpango huu wa miaka mitatu utawapatia vijana 300 wa Kitanzania kutoka familia zenye kipato cha chini ujuzi katika maeneo mbalimbali ya sekta ya kilimo, yakiwemo uzalishaji wa mazao, matengenezo ya vifaa, ufundi wa mitambo ya kilimo na stadi nyingine za kiufundi zinazohusiana na sekta hiyo. Mpango huu unalenga kuongeza uwezo wa vijana kupata ajira, kuhamasisha ujasiriamali na kuimarisha tija katika kilimo.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, TBL italipia gharama za mafunzo, huku VETA ikitoa mafunzo yaliyoidhinishwa, utaalamu wa kiufundi unaotambulika kitaifa. Washiriki pia watapata uzoefu wa vitendo katika shughuli za kilimo, ikiwemo fursa katika jamii za wakulima wa shayiri na mtama wanaoshirikiana na TBL.
Makubaliano hayo yalisainiwa na Michelle Kilpin, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, na CPA Anthony Kasore, Mkurugenzi Mkuu wa VETA.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Kasore alisisitiza umuhimu wa kukuza ujuzi unaoendana na mahitaji yanayobadilika ya sekta ya kilimo.
“VETA ilianzishwa ili kuwapatia Watanzania ujuzi wa vitendo unaoendana na mahitaji ya sekta mbalimbali za uzalishaji. Kadiri sekta yetu ya kilimo inavyoendelea kuwa ya kisasa, tunahitaji vijana wenye ujuzi ambao wanaweza kusaidia uzalishaji wa kilimo, kuboresha mbinu za kilimo, kutunza na kukarabati vifaa, pamoja na kutoa huduma muhimu za kiufundi. Ushirikiano huu unafungua fursa kwa vijana wenye vipaji ambao huenda wasiwe na uwezo wa kugharamia mafunzo, huku ukihakikisha kwamba ujuzi wanaoupata unakidhi mahitaji halisi ya sekta,” alisema Kasore.

Kilimo kinaendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania. Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2024, sekta hiyo ilichangia asilimia 26.3 ya pato la taifa; na kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, inaajiri zaidi ya nusu ya watu wote wanaofanya kazi nchini. Kadiri sekta hii inavyopiga hatua za kisasa, mahitaji ya ujuzi katika uzalishaji wa kilimo, umwagiliaji, usimamizi wa mazao baada ya kuvunwa, matumizi ya mitambo na huduma zinazohusiana nayo yanaendelea kuongezeka.
“Sehemu kubwa ya bidhaa tunazotengeneza huanzia katika mashamba ya Watanzania. Biashara yetu inakua sambamba na wakulima wanaotupatia malighafi, na mafanikio yao yanategemea upatikanaji wa ujuzi, teknolojia na huduma sahihi. Kwa kuwekeza kwa vijana wanaopata ujuzi wa vitendo katika kilimo, tunatengeneza fursa za ajira na ujasiriamali, huku tukiimarisha thamani inayowezesha watanzania kujipatia kipato na kuendeleza biashara yetu,” alisema Michelle Kilpin, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL.
Kwa mujibu wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, zaidi ya vijana 800,000 wa Kitanzania huingia katika soko la ajira kila mwaka. Mafunzo ya vitendo katika kilimo yanaweza kuwafungulia njia za kupata ajira, kujiajiri na kuanzisha biashara katika shughuli za kilimo, biashara za kilimo, matengenezo ya vifaa na huduma zinazohusiana nazo. Utafiti wa hivi karibuni wa VETA uliofuatilia hali ya wahitimu ulibaini kuwa asilimia 75 ya wahitimu walikuwa wameajiriwa au kujiajiri, huku kujiajiri kukiwa na sehemu kubwa zaidi kuliko ajira rasmi za kuajiriwa.
Ushirikiano huu unaendeleza uhusiano wa muda mrefu wa TBL na wakulima wa Tanzania ulioanza mwaka 1933. Kampuni hununua shayiri na mtama kutoka kwa wakulima wadogo zaidi ya 2,500 katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dodoma. Pia huwapatia mbegu, mafunzo ya kilimo na masoko ya uhakika.Pia TBL ilifanya uwekezaji kwenye uchakataji wa shayiri ndani ya nchi na Kiwanda chake cha Kilimanjaro Malting kilichopo Moshi kilikamilisha mwaka wake wa kwanza wa uzalishaji kamili mwaka 2025 kikitumia shayiri iliyolimwa nchini, hatua inayosisitiza dhamira ya TBL ya kuimarisha minyororo ya thamani ya kilimo cha ndani.
Akieleza kuhusu kuongezeka kwa nafasi ya VETA katika kukuza ujuzi, Kasore alisema idadi ya wanafunzi waliojiunga iliongezeka kutoka 69,347 mwaka 2022/23 hadi 116,468 mwaka 2025/26. Vyuo vipya 65 vinatarajiwa kufunguliwa Januari 2027.
“Kadiri VETA inavyopanua upatikanaji wa elimu ya ufundi stadi, ushirikiano na sekta ya uzalishaji ni muhimu katika kuziba pengo kati ya taasisi za mafunzo na mahitaji ya soko la ajira. Kupitia Ujuzi-Kwanza, tunawapatia vijana wa Kitanzania ujuzi wa vitendo unaoweza kuwawezesha kupata ajira, kufanya ujasiriamali na kujenga maisha endelevu. Kwa kushirikiana na TBL, tutafuatilia maendeleo ya wahitimu ili kupima matokeo ya mpango huu,” aliongeza Kasore.
Mpango huu unaendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, hususani malengo yake ya kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi, kuleta mageuzi katika kilimo na kukuza uchumi jumuishi. Pia unaunga mkono Ajenda ya 10/30, inayolenga ukuaji wa asilimia 10 kwa mwaka katika sekta ya kilimo ifikapo 2030, pamoja na programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow), inayohamasisha ushiriki wa vijana katika biashara za kilimo.
Akisisitiza matarajio ya muda mrefu ya mpango huo, Kilpin alisema:
“Hatutapima mafanikio kwa kuangalia tu idadi ya vijana waliopata mafunzo, bali pia kwa kuzingatia yale watakayofanikiwa kuyatimiza baada ya mafunzo. Lengo letu ni kuona vijana wa Kitanzania wakitumia ujuzi wa vitendo kujenga taaluma zenye manufaa, biashara zenye mafanikio na maisha endelevu, huku wakichangia kuimarisha sekta ya kilimo na kuongeza tija yake.”
Ujuzi-Kwanza: Kuwezesha Vijana, Kuimarisha Kilimo,Kukuza Tanzania.