×

Instagram Yazindua Mfumo Mpya wa Video Ndefu Mpaka Dakika 90

Baada ya kuiteka dunia kwa maudhui ya video fupi za wima (Reels), mtandao wa kijamii wa Instagram sasa unajiandaa kuchukua hatua nyingine kubwa, safari hii kuelekea upande tofauti kabisa.

Jukwaa hilo limezindua kipengele kipya kinachoitwa Features, kitakachowawezesha baadhi ya wabunifu wa maudhui kuchapisha video ndefu za mlalo (horizontal) zenye urefu wa hadi dakika 90.

Kiongozi Mkuu wa Instagram, Adam Mosseri, ametangaza kipengele hicho kwa kupost video ya dakika sita akiwa pamoja na Makamu wa Rais wa Bidhaa wa Instagram, Tessa Lyons.

Muundo huo mpya wa video unawalenga zaidi watayarishaji wa podcast, wachekeshaji na wabunifu wengine wa maudhui ya muda mrefu.

Kwa sasa, kipengele hicho kimeanza kupatikana kwa baadhi ya wabunifu wa maudhui nchini Marekani.

“Instagram inahusu kuwaunganisha watu kupitia ubunifu. Na ubunifu ni mpana zaidi kuliko video fupi pekee au kuchapisha picha nyingi katika chapisho moja,” alisema Lyons.

Kipengele cha Features kitafanya kazi sambamba na Reels, huku wabunifu wa maudhui wakiweza kuchapisha matangazo mafupi ya video zao ndefu kupitia Reels.

Watazamaji wataweza kufungua na kutazama video nzima kupitia matangazo hayo mafupi, kama Mosseri alivyoonesha pia kupitia akaunti yake ya Instagram.

“Kuanzia sasa, utaweza kuona kipande cha podcast unayoipenda, kisha kubofya ili kuendelea kuitazama au kutazama video nzima. Utaweza kufungua na kuona maudhui yote kwa sababu wabunifu wataweza kuunganisha Reels hizo na video zao kamili kupitia Features,” Lyons aliwaeleza watazamaji.

Hicho ni kimojawapo tu cha vipengele kadhaa vilivyotangazwa na Mosseri na Lyons. Instagram pia inapanga kuanzisha mfumo wa video wenye vipindi vingi, Series.

Kipengele hicho tayari kimeanza kujaribiwa kwa baadhi ya wabunifu wa maudhui nchini Marekani, India na Mexico, huku nchi nyingine zikitarajiwa kupata huduma hiyo hivi karibuni.

Aidha, Instagram inapanga kuunganisha matangazo ya moja kwa moja ya Instagram Live katika mtiririko wa Reels.

Hatua hiyo itaiwezesha mifumo ya Instagram kuanza kupendekeza matangazo ya moja kwa moja kama ilivyo kwa Youtube.

Leave a Comment