×

Watu Watatu Wafariki Baada ya Helikopta Mbili Kugongana Angani

Watu watatu wamefariki dunia baada ya helikopta mbili kugongana zikiwa angani karibu na Uwanja wa Ndege wa McMinnville, katika jimbo la Oregon, kaskazini magharibi mwa Marekani, Alhamisi, Oktoba 29, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Bodi ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri wa Marekani (NTSB), ajali hiyo ilihusisha helikopta aina ya Robinson R22 Beta na Airbus AS350B2, ambazo ziligongana majira ya saa 2:10 alasiri kwa saa za eneo hilo.

Baada ya kugongana, helikopta hizo zilianguka katika eneo la shamba binafsi karibu na Barabara Kuu ya 233, kulingana na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Sheriff ya Kaunti ya Yamhill.

Taarifa za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Marekani (FAA) zinaeleza kuwa helikopta moja ilikuwa na watu wawili, huku nyingine ikiwa na rubani mmoja. Hakuna aliyenusurika katika ajali hiyo.

Miongoni mwa waliofariki ni Maddie Aasbo, mwenye umri wa miaka 22, mkufunzi wa urubani kutoka Texas, pamoja na mwanafunzi wa urubani kutoka Uingereza ambaye jina lake halikutolewa wakati taarifa hizo zikitolewa ili kuruhusu familia yake kufahamishwa kwanza.

Mtu wa tatu aliyefariki ametambuliwa kuwa Tyler Delane Sturdevant, mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa Newberg, Oregon, aliyekuwa ndani ya helikopta aina ya Airbus AS350B2.

Kufuatia ajali hiyo, timu za uchunguzi kutoka NTSB na FAA zimefika eneo la tukio kuanza uchunguzi wa kubaini chanzo cha helikopta hizo kugongana.

NTSB imesema baada ya kurekodi na kuweka kumbukumbu za mabaki ya helikopta hizo, yatahamishiwa katika eneo maalumu lenye ulinzi kwa ajili ya uchunguzi wa kina.

Wakati huo huo, kampuni ya Jerry Trimble Helicopters imethibitisha kuwa moja ya helikopta zake ilihusika katika ajali hiyo, ikieleza kuwa inashirikiana kikamilifu na mamlaka husika katika uchunguzi.

Kampuni hiyo pia imetoa salamu za pole kwa familia za waliofariki na kuwashukuru waokoaji pamoja na huduma za dharura zilizofika eneo la tukio.

Hadi sasa, chanzo cha kugongana kwa helikopta hizo hakijabainishwa rasmi, huku uchunguzi ukiendelea chini ya mamlaka za usalama wa usafiri wa anga nchini Marekani.

Leave a Comment