×

Video: Spika Aagiza Viongozi Walionunua Magari ya Kifahari Kuitwa Bungeni

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, ametoa maagizo kwa watendaji na viongozi wa Serikali walionunua magari ya kifahari kinyume na maelekezo ya waraka wa Utumishi wa Umma kuitwa na kuhojiwa mbele ya kamati za Bunge.

Spika Zungu amesisitiza umuhimu wa Serikali kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kupunguza gharama zinazotokana na ununuzi wa magari ya gharama kubwa pamoja na matumizi ya mafuta katika taasisi za Serikali.

Ameeleza kuwa ni muhimu viongozi na watendaji wa umma kuzingatia miongozo iliyowekwa na Serikali kuhusu matumizi ya rasilimali za Taifa, badala ya kutumia fedha nyingi kununua magari ya kifahari yasiyoendana na sera ya kubana matumizi.

Aidha, Spika huyo amezitaka taasisi za umma kuanza kuangalia uwezekano wa kutumia magari yanayotumia teknolojia ya umeme na gesi, yakiwemo magari ya mfumo wa Hybrid, ili kupunguza gharama za uendeshaji na matumizi ya mafuta.

Katika kusisitiza hoja hiyo, Zungu ametolea mfano Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akipunguza misafara yake kama sehemu ya jitihada za kudhibiti matumizi ya Serikali.

Maelekezo hayo yanakuja wakati suala la uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma likiendelea kuwa sehemu muhimu ya mijadala kuhusu usimamizi wa rasilimali za Serikali.

Kwa hatua hiyo, viongozi na watendaji watakaobainika kukiuka waraka unaosimamia ununuzi wa magari wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi na kutoa maelezo mbele ya kamati husika za Bunge.

Leave a Comment