
Mwigizaji mkongwe wa Uingereza, Sir Patrick Stewart, aliyefahamika zaidi kupitia filamu na tamthilia za Star Trek na X-Men, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86.
Taarifa ya kifo chake imetolewa Alhamisi kupitia akaunti zake rasmi za mitandao ya kijamii, ikieleza kuwa alifariki Jumatano, Oktoba 28, 2026, akiwa nyumbani kwake jijini Los Angeles, Marekani, chini ya uangalizi wa mkewe, Sunny Ozell.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Stewart alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi magonjwa ya Alzheimer na Lewy Body Dementia, ambayo huathiri uwezo wa ubongo katika kumbukumbu, fikra na utendaji wa mwili.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa wakati wa kifo chake alikuwa amezungukwa na familia na marafiki, huku kukiwa na muziki wa moja kwa moja, sala, machozi na vicheko katika kumuaga mwigizaji huyo.
Stewart alianza safari yake ya uigizaji zaidi ya miaka 60 iliyopita, akijiunga na kundi la waigizaji la Royal Shakespeare Company mwishoni mwa miaka ya 1960 kabla ya kufanya vizuri katika maigizo ya jukwaani na baadaye kuingia kwenye filamu na televisheni.

Alipata umaarufu mkubwa kimataifa kupitia nafasi ya Kapteni Jean-Luc Picard katika mfululizo wa Star Trek: The Next Generation, ambapo alionekana katika vipindi 176 pamoja na filamu nne za mfululizo huo.
Katika miaka ya 2000, alizidi kujijengea jina baada ya kuigiza kama Professor Charles Xavier, maarufu kama Professor X, katika filamu za X-Men, akiwa mwigizaji mwenza na Ian McKellen.
Miongoni mwa kazi nyingine alizoshiriki ni Dune, Ted, Chicken Little, Robin Hood: Men in Tights, Family Guy na American Dad.

Katika maisha yake ya kisanii, Stewart alijinyakulia tuzo ya Grammy, huku akiteuliwa mara nne kuwania tuzo za Emmy na mara tatu za Golden Globe. Pia alishinda tuzo mbili za Olivier kutokana na kazi zake za jukwaani.
Mwaka 2023 alichapisha kitabu cha kumbukumbu za maisha yake kilichoitwa Making It So, kikielezea safari yake ndefu katika tasnia ya burudani.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu na televisheni, hasa kwa mashabiki wa Star Trek na X-Men waliomfahamu kupitia wahusika wake waliodumu kwa miaka mingi.
Sir Patrick Stewart amefariki akiwa na miaka 86, lakini kazi zake na mchango wake katika tasnia ya burudani vitaendelea kukumbukwa na vizazi mbalimbali.
View this post on Instagram