Kijana mwenye umri wa miaka 24 nchini China amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya maelfu ya watu asiowafahamu kujitokeza kuhudhuria harusi yake leo Oktoba 31, 2026 kufuatia mwaliko alioutoa kupitia mitandao ya kijamii.
Xiao Xiao Xu, mkazi wa Zhaotong, Mkoa wa Yunnan, nchini China, aliamua kuwaalika watu asiowafahamu kwenye harusi yake baada ya kuwa na hofu kuwa sherehe hiyo isingekuwa na wageni wa kutosha kutokana na kukosa ndugu wengi wa karibu.
Xiao alipoteza baba yake akiwa na umri wa miaka mitatu, huku mama yake akiolewa tena miaka miwili baadaye. Alipofikisha umri wa miaka saba, pia alimpoteza bibi yake, hali iliyomfanya kukulia katika mazingira magumu akitegemea zaidi msaada wa kaka yake mkubwa.
Kutokana na changamoto za maisha, aliacha shule akiwa bado katika elimu ya sekondari ya chini na kuanza kufanya kazi mbalimbali ikiwemo ujenzi na udereva wa usafirishaji. Katika kipindi cha miaka kadhaa, alifanikiwa kuweka akiba ya Yuan 160,000 za China kwa ajili ya kugharamia harusi yake na msichana anayempenda, Chuichui.
Hata hivyo, kadiri siku ya harusi ilivyokuwa ikikaribia, alianza kuwa na wasiwasi kuhusu idadi ya wageni watakaohudhuria, akihofia kuwa ndugu zake wasingetosha kujaza hata meza tatu za wageni.
Kutokana na hali hiyo, Xiao aliamua kutumia mitandao ya kijamii kutoa mwaliko wa kipekee kwa watu mbalimbali, akiwaomba wajitokeze nyumbani kwake kusherehekea siku yake ya ndoa.
Kwa mshangao wake, mwaliko huo ulisambaa kwa kasi na kuwafikia maelfu ya watu kutoka maeneo mbalimbali, huku wakazi wa kijiji chake pamoja na watu asiowafahamu wakijitokeza kwa wingi kuunga mkono harusi hiyo.

Msaada uliotolewa haukuishia kwenye kuhudhuria pekee, kwani baadhi ya watu walijitolea kupika chakula cha wageni, wengine wakaleta vyakula na mahitaji mbalimbali yaliyohitajika kufanikisha sherehe hiyo.
Aidha, watu mbalimbali walijitolea magari ya harusi, huku mmoja wao akitoa gari aina ya Maybach kwa ajili ya maharusi.
Wengine walishiriki kupamba nyumba na kuandaa mazingira ya sherehe, ikiwemo kutoa mishumaa ya harusi.
Watu wema bado wanaishi 🎉