
Taasisi ya Tanlink Medical Tourism Agency (TANLINK) imezindua programu tumishi (Good Doctor App), inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kuwaunganisha wagonjwa na madaktari pamoja na kuwawezesha kuweka miadi ya matibabu katika hospitali kupitia simu za mkononi, bila kujali mahali walipo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANLINK, Dkt. Hassan Fyumagwa, amesema Good Doctor App ni sehemu ya mapinduzi ya teknolojia katika sekta ya afya, yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma na kurahisisha maisha ya wananchi.
Amesema ujio wa programu hiyo unaendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kuboresha mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi.
Dkt. Fyumagwa amesema kupitia Good Doctor App, wagonjwa sasa wataweza kupunguza usumbufu wa kusubiri kwenye foleni hospitalini kwa kuweka miadi na madaktari moja kwa moja kupitia simu zao za mkononi.
Ameongeza kuwa programu hiyo inampa mtumiaji uhuru wa kuchagua hospitali anayotaka kupata huduma pamoja na kupanga miadi ya matibabu akiwa mahali popote.
“Uzinduzi wa App hii unaenda sambamba na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
“Sasa mgonjwa anaweza kupunguza usumbufu wa foleni hospitalini kwa kuweka miadi (appointment) na daktari moja kwa moja kupitia App hii, lakini pia hii inampa mteja uwezo wa kuchagua hospitali na huduma popote alipo,” amesema Dkt. Fyumagwa.
Kwa mujibu wa TANLINK, Good Doctor App tayari inapatikana kwa watumiaji wa simu za iPhone kupitia App Store, pamoja na simu zinazotumia mfumo wa Android kupitia Google Play Store.
Uzinduzi wa programu hiyo unatarajiwa kuongeza matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya kwa kurahisisha mawasiliano kati ya wagonjwa, madaktari na hospitali, huku ukiwapa wananchi fursa ya kupanga huduma zao za matibabu kwa urahisi zaidi.