
AGL Tanzania imechukua hatua muhimu katika kulinda mazingira kwa kutekeleza mpango wake wa “Plastic-Less”, unaolenga kupunguza matumizi ya plastiki zinazotumika mara moja na kuhamasisha matumizi ya njia mbadala endelevu.
Kupitia mpango huo, kampuni iligawa chupa za maji zinazoweza kutumika tena kwa wafanyakazi wake wote ili kupunguza matumizi ya chupa za plastiki zinazotupwa baada ya matumizi. Aidha, visambaza maji viliwekwa katika vyumba vya mikutano na maeneo mbalimbali ya kazi ili kurahisisha upatikanaji wa maji na kuwahamasisha wafanyakazi kujaza tena chupa zao badala ya kutumia plastiki za matumizi ya mara moja.
Kwa wageni wanaotembelea kampuni, AGL imeanzisha matumizi ya glasi za maji zinazoweza kuoshwa na kutumika tena, hatua inayochangia zaidi kupunguza taka za plastiki na kuimarisha usimamizi wa mazingira.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Meneja wa Masuala ya Sheria, AGL, Angeline Mtulia alisema“Uendelevu ni ahadi yetu kama kampuni na ni wajibu tunaoshirikiana na wafanyakazi wetu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Kupitia mpango wa ‘Plastic-Less’, tumeonesha kwamba mabadiliko madogo ya tabia, yanapoungwa mkono na miundombinu sahihi pamoja na ushirikiano wa kijamii, yanaweza kuleta matokeo yenye manufaa makubwa kwa mazingira na jamii.”
Uzinduzi rasmi wa mpango huo ulifanyika tarehe 5 Juni, sambamba na maadhimisho ya juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi chini ya kaulimbiu ya “Act Now for the Climate”. Katika hafla hiyo, timu ya QHSE ilitoa elimu kuhusu malengo ya mpango huo na umuhimu wa kila mfanyakazi kushiriki katika kufanikisha utekelezaji wake.

Sehemu ya shughuli hizo ilihusisha mafunzo ya uhamasishaji kuhusu usimamizi wa taka na uhifadhi wa mazingira yaliyotolewa kwa ushirikiano na kundi la urejelezaji taka la The Recyclers. Kupitia mafunzo hayo, wafanyakazi walielimishwa kuhusu athari za matumizi ya plastiki kwa mazingira na umuhimu wa kubadili tabia ili kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Mbali na juhudi za ndani ya kampuni, AGL kupitia kampuni dada ya EALS ilipanua mpango huo kwa jamii kupitia shughuli za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). Kampuni hizo zilitembelea Shule ya Sekondari Mabibo na kutoa mapipa 12 ya kuhifadhia taka, vizima moto 27 pamoja na king’ora cha tahadhari ya moto.
Ziara hiyo ililenga kuimarisha usimamizi wa mazingira na usalama shuleni huku ikiendeleza ushirikiano uliopo kati ya kampuni na shule hiyo, uliotokana na miradi mingine ya maendeleo iliyotekelezwa mwaka 2025 ikiwemo ujenzi wa vyoo na maktaba.
Wanafunzi wa shule hiyo walipata mafunzo kuhusu madhara ya matumizi ya plastiki na umuhimu wa kutunza mazingira. Pia walijifunza namna sahihi ya kutenganisha taka kwa kutumia mapipa yaliyowekwa alama maalum kwa ajili ya taka za chakula, plastiki na taka nyinginezo.
Aidha, mafunzo ya usalama wa moto yalisisitizwa, yakikamilisha juhudi za muda mrefu zinazofanywa na Jeshi la Zimamoto katika kuwaelimisha wanafunzi kuhusu namna ya kujikinga na majanga ya moto.
Kwa mujibu wa AGL, mafanikio ya mpango wa “Plastic-Less” yataendelea kufuatiliwa kwa kupima kiwango cha matumizi ya plastiki kabla na baada ya utekelezaji wake. Hatua hiyo itasaidia kutathmini mchango wa mpango huo katika kupunguza taka za plastiki na kulinda mazingira.
Kupitia mpango huu, AGL Tanzania imeonesha dhamira yake ya kuunga mkono Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa kuunganisha uhifadhi wa mazingira, usimamizi bora wa rasilimali na maendeleo ya jamii. Mpango huo umeacha athari chanya kwa wafanyakazi na jamii, huku ukiendelea kujenga utamaduni wa uwajibikaji na uendelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.