
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amewaelekeza ndugu zake kuhakikisha kaka yake, Wakili Alute Mughwai Lissu, anazikwa kwa heshima na staha, huku akiahidi kuchangia Shilingi milioni 15 kwa ajili ya kugharamia shughuli za mazishi hayo.
Lissu, ambaye kwa sasa yupo mahabusu katika Gereza la Ukonga akisubiri hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili inayotarajiwa kutolewa Novemba 6, 2026, alipokea taarifa za kifo cha kaka yake Novemba 1, mwaka huu, baada ya kutembelewa na ndugu zake gerezani.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, mdogo wake Lissu, Ikota Lissu, amesema amemfikishia kaka yao taarifa za msiba huo ilikuwa kazi ngumu kihisia kutokana na ukaribu mkubwa uliokuwepo baina yake na marehemu.
Amesema marehemu Alute alikuwa mtu muhimu katika maisha ya Tundu Lissu, hasa katika masuala ya sheria na siasa, ambapo alikuwa mshauri na mlezi wake mkuu.
Kwa mujibu wa Ikota, baada ya kupokea taarifa hizo, Tundu Lissu aliisisitiza familia kuhakikisha inashirikiana kwa karibu na viongozi wa Kanisa Katoliki mkoani Singida pamoja na marafiki wa marehemu ili maandalizi ya mazishi yafanyike kwa utulivu na heshima inayostahili.
Wakili Alute Mughwai Lissu alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 1, 2026, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Selian.
Mazishi ya marehemu yamepangwa kufanyika katika Kijiji cha Mahambe, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, huku familia ikitarajia kukamilisha maandalizi baada ya kutolewa kwa hukumu ya kesi inayomkabili Tundu Lissu Novemba 6, 2026.
Taarifa za msiba huo zimeibua huzuni kwa ndugu, jamaa na watu waliokuwa karibu na familia hiyo, kutokana na nafasi aliyokuwa nayo marehemu katika maisha ya familia na jamii.