
WAKATI mashabiki wa muziki wakiendelea kuwalinganisha Mrembo anayefanya vizuri kwenye anga la Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ na Malkia wa muziki wa Kizazi Kipya nchini Tanzania, Zuhura Othman Soud, maarufu kama Zuchu, kuhusu nani mwenye mafanikio makubwa zaidi, safari zao zinaibua mjadala mpana unaozidi idadi ya mashabiki, watazamaji wa YouTube na umaarufu wa mitandaoni.

Katika tasnia ya muziki, mafanikio hayaishii kwenye kutoa nyimbo zinazofanya vizuri, kujaza matamasha au kuwa na mamilioni ya wafuasi kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa wasanii wa kizazi cha sasa, uwezo wa kujenga biashara, kumiliki lebo, kuwekeza na kuanzisha mifumo inayoweza kuendelea kuingiza kipato nje ya muziki ni sehemu muhimu ya kupima mafanikio.
Katika eneo hilo, Nandy, anayefahamika pia kama The African Princess, ana safari inayostahili kuangaliwa kwa jicho tofauti.
Hata hivyo, hilo halimaanishi kuwa Zuchu hana mafanikio yake. Msanii huyo naye amejijengea jina kubwa ndani na nje ya Tanzania, akitumia muziki na ushirikiano wa kibiashara kujenga chapa yake.
SAFARI ZAO ILIVYOANZA
Nandy na Zuchu wana historia inayogusana tangu waliposhiriki mashindano ya TECNO Own The Stage mwaka 2015 nchini Nigeria.
Nandy alifanikiwa kushika nafasi ya pili katika mashindano hayo, hatua iliyomfungulia milango ya kujenga jina lake katika muziki wa Afrika Mashariki. Mwaka 2016 aliingia rasmi kwenye soko la muziki kupitia wimbo wake Nagusagusa.

Kwa upande wa Zuchu, jina lake lilipata umaarufu mkubwa zaidi mwaka 2020 baada ya kusainiwa na lebo ya WCB Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platnumz.
Alitambulishwa rasmi sokoni kupitia EP yake ya I Am Zuchu, iliyokuwa mwanzo wa safari yake kubwa katika muziki.
Tofauti ya mazingira hayo ya kazi imekuwa sehemu muhimu ya mjadala kuhusu safari zao, hasa katika suala la umiliki na uendeshaji wa biashara ya muziki.

NANDY NA UMILIKI WA LEBO YAKE
Moja ya hatua kubwa katika safari ya Nandy ni kuanzisha lebo yake ya muziki, The African Princess Label, mwaka 2023.
Kupitia lebo hiyo, Nandy alijitanua kutoka kuwa msanii anayefanya muziki wake pekee hadi kuwa mtu anayeshiriki katika kukuza na kusimamia vipaji vya wasanii wengine.
Miongoni mwa wasanii walioingia kwenye mfumo huo ni Yammi, ambaye alianza safari yake kupitia EP ya Three Hearts.

Hatua hii inampa Nandy nafasi mbili ndani ya tasnia: kuwa msanii anayezalisha kazi zake na wakati huohuo kuwa mmiliki wa biashara inayoweza kuwekeza katika vipaji vingine.
Kwa upande wa Zuchu, yeye ni msanii aliyesainiwa chini ya WCB Wasafi. Hivyo, tofauti inayoweza kuonekana hapa ni kwamba Nandy ameanzisha na kuendesha lebo yake, wakati Zuchu anafanya kazi ndani ya mfumo wa lebo ambayo hakumiliki.
Ni tofauti ya kimuundo inayopaswa kuzingatiwa wakati wa kuchambua safari zao, bila kupuuza mafanikio ambayo kila mmoja ameyapata katika mazingira yake.

MITANDAO YA KIJAMII: NANDY ANAONGOZA INSTAGRAM, ZUCHU TIKTOK NA YOUTUBE
Katika zama ambazo mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya biashara ya muziki, idadi ya wafuasi inaweza kuonyesha ukubwa wa ushawishi wa msanii katika jukwaa husika.
Mpaka leo Novemba 4, 2026, Nandy amefikisha wafuasi milioni 10.7 Instagram, huku Zuchu akiwa na milioni 7.6.
Hata hivyo, hali ni tofauti katika majukwaa mengine.
Zuchu anaongoza TikTok akiwa na takribani wafuasi milioni saba, dhidi ya milioni 2.7 wa Nandy.
Katika YouTube, Zuchu naye anaongoza kwa kuwa na subscribers takribani milioni tano, wakati Nandy akiwa na milioni 1.9.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa kila msanii ana eneo ambalo amejijengea nguvu zaidi. Nandy ana ushawishi mkubwa Instagram, huku Zuchu akiwa na ukubwa mkubwa zaidi TikTok na YouTube.

ALBAMU NA KAZI ZILIZOJENGA MAJINA YAO
Nandy amekuwa na safari ndefu katika utoaji wa kazi za muziki. Mwaka 2018 alitoa albamu yake ya The African Princess, iliyosaidia kuimarisha utambulisho wake katika soko la muziki.
Baadaye aliendelea kutoa EP mbalimbali zikiwemo Taste, Maturity na Wanibariki, huku akiendelea kujenga chapa yake kupitia jina la The African Princess.
Kwa upande wa Zuchu, EP yake ya I Am Zuchu ya mwaka 2020 ilikuwa hatua muhimu katika kumtambulisha rasmi kwa mashabiki. Kupitia kazi hiyo na nyimbo zilizofuata, aliweza kujenga nafasi yake katika muziki wa Tanzania na Afrika Mashariki.
Tofauti kubwa hapa ni namna kila mmoja alivyojenga chapa yake. Nandy ameifanya The African Princess kuwa sehemu ya utambulisho wake wa kisanii na kibiashara, huku Zuchu akijijengea jina lake ndani ya mfumo wa WCB Wasafi.

YOUTUBE: ZUCHU ANA NGUVU KUBWA YA WATAZAMAJI
Licha ya Nandy kuwa na mafanikio katika umiliki wa lebo na biashara, Zuchu ana takwimu kubwa zaidi katika upande wa watazamaji wa YouTube.
Kwa mujibu wa takwimu zilizoripotiwa Novemba 2025, Zuchu alikuwa amefikisha zaidi ya watazamaji bilioni moja katika video zake, wakati Nandy akiwa na zaidi ya milioni 306.
Takwimu zilizotajwa za Novemba 2026 zinaonyesha Zuchu akiwa amefikisha zaidi ya watazamaji bilioni 1.3 kwenye chaneli yake, huku Nandy akiwa na zaidi ya milioni 375.

Hizi ni takwimu zinazoonyesha ukubwa wa matumizi ya kazi za Zuchu kwenye jukwaa hilo la kidijitali.
Kwa upande wa biashara ya muziki, watazamaji wengi wanaweza kuongeza thamani ya chapa ya msanii kupitia matangazo, usambazaji wa kazi na fursa mbalimbali za kibiashara.
Hivyo, mafanikio ya Zuchu kwenye YouTube ni sehemu muhimu ya mjadala huu na hayawezi kupuuzwa.

NANDY: MUZIKI KAMA CHANZO CHA KUJENGA BIASHARA
Moja ya mambo yanayovutia katika safari ya Nandy ni namna ambavyo amejaribu kupanua shughuli zake nje ya muziki.
Mbali na The African Princess Label, amekuwa akihusishwa na biashara ya vipodozi kupitia chapa ya Shushi Products.
Pia amehusishwa na biashara ya malazi kupitia Naya Villa, inayotangaza huduma za nyumba za kifahari za kupangisha kwa muda mfupi.
Hizi ni shughuli zinazoonyesha namna wasanii wanavyoweza kutumia umaarufu wao kujenga biashara katika sekta nyingine.
Nandy pia ameendesha tamasha lake la Nandy Festival, ambalo limekuwa jukwaa la kukutanisha wasanii, burudani na kukuza vipaji mbalimbali.
Kwa hatua hiyo, ameongeza nafasi yake ndani ya tasnia kutoka kuwa mtu anayehusika na utengenezaji wa muziki hadi kuwa sehemu ya uandaaji wa majukwaa ya burudani.

MAGARI NA MALI ZA NANDY
Katika upande wa mali binafsi, Nandy amewahi kuhusishwa na umiliki wa magari mbalimbali ya kifahari.
Taarifa zilizochapishwa na Global Publishers mwaka 2019 na 2021 zilimtaja kuwa na magari yakiwemo, Range Rover Evoque, Land Rover Discovery, BMW X1, Mercedes-Benz E-Class, Toyota Alphard, Toyota Harrier na Toyota Noah na kwa sasa anamiliki Mercedes-Benz AMG G63 (G-Wagon) Linatajwa kuwa na thamani kuanzia Milioni 600 hadi Milioni 800 za Kitanzania (TSh 600M – 800M+).
Hata hivyo, taarifa hizo ni za miaka iliyopita na hazithibitishi kuwa magari yote hayo bado yako chini ya umiliki wake.
Pia Nandy aliwahi kuripotiwa kuwazawadia wazazi wake nyumba, hatua iliyotajwa kuwa sehemu ya mafanikio yake na namna alivyotumia matunda ya kazi yake kuwasaidia watu wa karibu.
Ni muhimu kutofautisha taarifa za mali zilizowahi kuripotiwa na thamani halisi ya utajiri wa mtu, ambayo inahitaji nyaraka na taarifa za kifedha zilizothibitishwa.

ZUCHU NAYE ANAVYOJENGA MAISHA NJE YA MUZIKI
Kwa upande wa Zuchu, mafanikio yake hayaishii kwenye muziki pekee. Tangu alipoingia rasmi kwenye soko mwaka 2020, ameendelea kujijengea thamani kupitia kazi za muziki na mikataba ya kibiashara.
Mwaka 2021 Zuchu alikuwa amekataa mkataba wa matangazo ya pombe uliokuwa na thamani ya Sh milioni 250.
Pia amekuwa akihusishwa na ushirikiano wa kibiashara na chapa mbalimbali, zikiwemo Darling Hair na Tridea Cosmetics.
Katika upande wa magari, Zuchu aliwahi kujinunulia Range Rover mwaka 2023.
Pia anahusishwa kuendesha au kutumia magari ya kifahari kupitia familia na mpenzi wake Diamond Platnumz, kama vile Range Rover na mara kwa mara kuonekana akitumia au kupanda magari ya kifahari ya WCB kama Cadillac Escalade ya Diamond Platnumz.
Novemba 2026, Zuchu alitangaza kujinunulia Bentley Continental GT V8 Azure, akieleza kuwa gari hilo lilikuwa ndoto yake ya muda mrefu na mafanikio yaliyotokana na muziki.
Pia mwaka 2025 alionyesha nyumba ya vyumba vitano aliyokuwa akiijenga kwa ajili ya mama yake, Khadija Kopa, ikiwa ni sehemu ya kutimiza ndoto yake ya kumzawadia mzazi wake makazi bora.
Taarifa nyingine za mwaka 2026 zimemhusisha na uwekezaji wa vyumba viwili vya kifahari Zanzibar, ingawa umiliki na thamani ya uwekezaji huo vinahitaji uthibitisho wa ziada.
Mafanikio hayo yanaonyesha namna Zuchu naye anavyotumia muziki na chapa yake kujenga maisha na kupanua vyanzo vya mapato.

NANDY NA ZUCHU: NANI ANAPASWA KUHESHIMIWA ZAIDI?
Kwa kuangalia safari zao, ni wazi kuwa Nandy na Zuchu wana mafanikio katika maeneo tofauti.
Nandy ana historia ndefu zaidi katika muziki, ameanzisha lebo yake, amejihusisha na biashara ya vipodozi na malazi, ameandaa tamasha lake na kuendelea kujenga chapa ya The African Princess.
Kwa upande mwingine, Zuchu ana mafanikio makubwa katika YouTube na TikTok, amejenga ushawishi mkubwa wa kidijitali, amefanya mikataba ya kibiashara na kuonyesha mafanikio yake kupitia ununuzi wa mali mbalimbali.

Hata hivyo, kuna jambo moja ambalo mara nyingi husahaulika katika mijadala ya aina hii: si kila msanii ana safari inayofanana na ya mwingine.
Nandy amekuwa akijenga mfumo wake wa biashara na lebo yake, wakati Zuchu amefanya safari yake kubwa ndani ya mfumo wa WCB Wasafi, ambao umekuwa na mchango katika kukuza kazi zake.
Hiyo haimaanishi kuwa mafanikio ya mmoja yanapaswa kupunguza thamani ya mwingine.
Lakini pia, kumlinganisha Nandy na Zuchu kwa kuangalia followers, views au umaarufu pekee ni kuacha nje sehemu muhimu ya safari ya Nandy, hususan katika umiliki wa biashara na kujenga mifumo ya kukuza vipaji vingine.
Kwa kweli, mafanikio ya msanii hayapaswi kupimwa kwa idadi ya magari, nyumba au watazamaji pekee. Yanapaswa pia kuangaliwa kwa uwezo wa kujenga chapa, kumiliki biashara, kuwekeza, kutengeneza ajira na kuacha mfumo utakaoweza kuendelea kufanya kazi hata pale msanii anapokuwa hayupo jukwaani.
MAISHA YA MAPENZI: NANDY NA BILLNASS, ZUCHU NA DIAMOND
Mbali na mafanikio ya muziki na biashara, maisha yao binafsi pia yamekuwa sehemu ya mijadala ya mashabiki.
Nandy yupo kwenye ndoa na msanii mwenzake, Billnass, ambaye pia ni sehemu ya tasnia ya muziki. Muunganiko wao umekuwa ukivutia kutokana na namna wanavyounganisha maisha ya familia na shughuli zao za kisanii na kibiashara.
Kwa upande wa Zuchu, amekuwa akihusishwa kimapenzi na Diamond Platnumz, ambaye ni mmiliki wa WCB Wasafi, lebo anayoifanyia kazi. Uhusiano wao umekuwa ukivuta hisia za mashabiki na kuendelea kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, maisha ya mapenzi ya wasanii hayapaswi kuwa kipimo pekee cha mafanikio yao. Kilicho muhimu zaidi ni kutambua kazi, juhudi, uwekezaji na mchango ambao kila mmoja ameutoa katika tasnia ya burudani.
Kwa hiyo, kumlinganisha Nandy na Zuchu si tatizo lenyewe, lakini kumhukumu Nandy kwa vigezo vya umaarufu wa mitandaoni pekee ni kupuuza sehemu kubwa ya safari yake. Nandy ana historia yake, uwekezaji wake na mfumo wake alioujenga kwa miaka mingi. Zuchu naye ana mafanikio yake yanayostahili kutambuliwa.
Mwisho wa siku, muziki si mashindano ya nani ana followers wengi, bali pia ni uwezo wa kutumia kipaji kujenga biashara, kuwekeza na kuacha alama ndani ya tasnia.
STORI NA GLOBAL DIGITAL NA MTANDAO