Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, amepinga maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuhusu gharama za ujenzi wa Uwanja wa Arusha unaokadiriwa kufikia Shilingi bilioni 338.
Baba Levo amesema hoja ya kuutetea Uwanja wa Arusha kwa kuulinganisha na mapungufu ya Uwanja wa Benjamin Mkapa haina mashiko, akisisitiza kuwa viwanja vyote vinasimamiwa na wizara moja.
Akizungumza na Jambo TV kuhusu ufafanuzi wa Serikali uliotolewa Bungeni, mbunge huyo amesema hapingi ujenzi wala ubora wa Uwanja wa Arusha, bali anataka kuwepo kwa uwazi kuhusu matumizi ya fedha za umma.
Amesisitiza kuwa ndiyo sababu ameomba Serikali iwasilishe mchanganuo wa gharama za mradi huo, unaojulikana kama Bill of Quantities (BOQ), ili kuwezesha kufahamu namna fedha hizo zilivyopangwa na kutumika.
“Huwezi kuutetea Uwanja wa Arusha kwa kuuponda wa Mkapa na viwanja vyote vipo kwenye Wizara yako. Sisi hatujakataa kiwanja cha Arusha siyo bora ila tumehoji kuhusu matumizi ya pesa, mwisho tumeomba BOQ,” amesema Baba Levo.
Hoja hiyo aliitoa pia Bungeni jijini Dodoma Novemba 4, 2026, alipolinganisha gharama za Uwanja wa Arusha unaotarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 na Uwanja wa Benjamin Mkapa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000.
Kwa mujibu wa hoja yake, Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliokamilishwa kati ya mwaka 2005 na 2007, uligharimu kati ya Shilingi bilioni 40 na 63, huku Uwanja wa Arusha ukikadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 338.
Aidha, Baba Levo alirejelea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akidai kuwa mkandarasi wa mradi wa Uwanja wa Arusha alipatikana kupitia mfumo wa manunuzi wa Single Source, hali aliyoihusisha na ongezeko la gharama za mradi.
Hata hivyo, Waziri Makonda alipojibu hoja hizo Bungeni alieleza kuwa Uwanja wa Arusha hauwezi kulinganishwa moja kwa moja na Uwanja wa Benjamin Mkapa kutokana na tofauti za miundombinu na viwango vilivyotumika.
Makonda alitolea mfano changamoto ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kushindwa kutumika kwa michezo wakati wa mvua kubwa, akisema Uwanja wa Arusha umezingatia mahitaji ya miundombinu ya kisasa.
Kuhusu gharama, Waziri huyo alifafanua kuwa kiasi cha Shilingi bilioni 338 kinajumuisha takribani Shilingi bilioni 52 za kodi, huku makadirio ya awali ya Shilingi bilioni 107 yakiwa hayajajumuisha kodi hiyo.
Aliongeza kuwa ongezeko la gharama limetokana na mabadiliko ya usanifu na kuboresha miundombinu kufikia viwango vya kimataifa vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ikiwemo ujenzi wa Sky Boxes 21 pamoja na lifti sita.
Kuhusu matumizi ya mfumo wa Single Source, Makonda alisema mfumo huo unatambulika kisheria na unaweza kutumika katika taratibu za manunuzi ya umma.
Hadi sasa, hoja kuu katika mjadala huo inaendelea kuwa uwazi wa gharama za mradi, mchanganuo wa matumizi ya fedha na sababu za tofauti kubwa kati ya makadirio ya awali na gharama ya mwisho ya ujenzi wa Uwanja wa Arusha.