×

Eisenkot Aanza Kumpa Presha Netanyahu, Apanga Kufuta Mabadiliko Yake Ya Kisheria

Kiongozi wa kisiasa nchini Israel, Gadi Eisenkot, ameahidi kubadili sera kadhaa za Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kufuatia kuapishwa kwa Bunge jipya la nchi hiyo, hatua inayofungua ukurasa mpya wa mabadiliko ya kisiasa na kiutawala nchini humo.

Eisenkot, ambaye ni jenerali wa zamani wa jeshi la Israel, amepewa jukumu la kuunda serikali mpya ndani ya kipindi cha hadi wiki sita, huku wapinzani wa Netanyahu wakiwa na idadi kubwa ya wabunge katika Bunge jipya linalojulikana kama Knesset.

Mchakato huo unaweza kumaliza utawala wa Netanyahu, ambaye amekuwa waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Israel.

Katika siku ya kwanza ya shughuli za Bunge jipya, muungano unaoongozwa na Eisenkot uliwasilisha miswada kadhaa inayolenga kubadili sera za serikali inayoondoka madarakani.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuanzisha uchunguzi rasmi wa serikali kuhusu mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7, 2023, kuweka ukomo wa muda wa mtu kushikilia nafasi ya waziri mkuu na kufuta mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na serikali ya Netanyahu ambayo yalipunguza mamlaka ya mahakama.

Hata hivyo, bado haijafahamika ni kwa kasi gani miswada hiyo itajadiliwa na kupitishwa katika Bunge hilo.

Akizungumza kabla ya hafla ya kuapishwa kwa wabunge, Eisenkot alisema serikali anayokusudia kuunda itakuwa ya wananchi wote wa Israel, bila kujali waliunga mkono chama chake au la.

Alisema dhamira yake ni kujenga serikali ambayo wananchi wote wanaweza kuiamini na inayowakilisha maslahi ya taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Netanyahu ameendelea kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyomnyima muungano wake wingi wa wabunge, huku akitoa madai kwamba vyama vinavyoongozwa na Waarabu viliiba uchaguzi, bila kutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa kwa Bunge jipya, Netanyahu alikosoa viongozi wa upinzani wanaoonyesha utayari wa kushirikiana na vyama vya Waarabu katika kuunda serikali.

Alisema Israel inakabiliwa na changamoto za kiusalama zinazohitaji vyama vya Kiyahudi kuungana, akitaja tishio linalotokana na Iran.

Hata hivyo, Eisenkot alikosoa hotuba hiyo na kuitaja kuwa ya kugawanya wananchi na kuchochea chuki. Alisema kauli za Netanyahu zimemshawishi zaidi kwamba hafai kuendelea kushikilia wadhifa wa waziri mkuu.

Kutokana na mvutano huo, Eisenkot alitangaza kufuta mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika Jumatano na chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu.

Wakati huohuo, wapinzani wa Netanyahu wameanza hatua za kubadili uongozi wa Bunge kwa kuwasilisha saini za wabunge wanaotaka Spika wa sasa, Amir Ohana, aondolewe madarakani.

Muungano wa upinzani umependekeza jina la Matan Kahana, mwanachama mwandamizi wa chama cha Yashar cha Eisenkot, kushika nafasi hiyo.

Nafasi ya Spika wa Bunge ina umuhimu mkubwa kwa sababu ndiye anayeamua miswada itakayowasilishwa na kujadiliwa, hivyo uteuzi wa kiongozi anayeungwa mkono na upinzani unaweza kurahisisha utekelezaji wa ajenda yao ya kisiasa.

Pamoja na kuanza kwa Bunge jipya, Netanyahu na baraza lake la mawaziri wataendelea kuongoza serikali kwa muda wa mpito wakati Eisenkot akiendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama mbalimbali ili kupata muungano wa kutosha kuunda serikali.

Iwapo Eisenkot atashindwa kuunda serikali ndani ya muda uliowekwa, Rais wa Israel, Isaac Herzog, anaweza kumpa Netanyahu nafasi nyingine ya kujaribu kuunda serikali.

Netanyahu pia anaendelea kukabiliwa na kesi ya rushwa mahakamani, pamoja na uwezekano wa kukabiliwa na uchunguzi kuhusu mapungufu ya kiusalama yaliyotangulia mashambulizi ya Oktoba 7, 2023.

Mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea Israel yanafuatiliwa kwa karibu kutokana na athari zake zinazoweza kujitokeza katika sera za ndani, usalama wa taifa na uhusiano wa nchi hiyo na mataifa ya Mashariki ya Kati, hususan Iran.

Leave a Comment