
Idadi ya watu waliofariki dunia kufuatia kuporomoka kwa jengo la makazi katika eneo la Flatbush, Brooklyn, jijini New York, Marekani, imeongezeka na kufikia wanane, huku wengine wasiopungua 19 wakijeruhiwa na hofu ya idadi hiyo kuongezeka ikiendelea kutokana na uwezekano wa watu wengine kunasa chini ya vifusi.
Jengo hilo lenye ghorofa tatu liliporomoka majira ya saa 10 jioni Jumatano, Novemba 11, 2026, likiwafunika wakazi pamoja na baadhi ya wafanyakazi waliokuwa katika eneo la ujenzi lililo jirani. Operesheni za uokoaji zinaendelea huku zaidi ya wahudumu 250 wa zimamoto na huduma za dharura wakishiriki katika zoezi hilo.

Taarifa zinaeleza kuwa jengo hilo lilijengwa mwaka 1930 na lilikuwa na historia ya ukiukwaji wa viwango vya usalama, ambapo kumbukumbu za mamlaka ya makazi jijini New York zinaonesha kuwa lilikuwa limewekewa jumla ya ukiukwaji wa kanuni 98 tangu mwaka 1972.
Miongoni mwa dosari zilizobainika mwaka 2026 pekee ni pamoja na hitilafu za mifumo ya huduma, paa lililoharibika, uwepo wa kunguni pamoja na kukosekana kwa vifaa vya tahadhari dhidi ya moto na gesi ya Carbon Monoxide.

Mamlaka bado hazijathibitisha chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo, lakini uchunguzi unatarajiwa kuangalia shughuli za uchimbaji zilizokuwa zikiendelea katika eneo la ujenzi lililopakana na jengo hilo.
Taarifa zinaeleza kuwa eneo hilo lilikuwa limepangwa kujengwa jengo la makazi lenye ghorofa tisa, likiwa na nyumba 64 pamoja na supermarket. Hata hivyo, mamlaka zilikuwa zimetoa agizo la kusimamisha shughuli za ubomoaji katika eneo hilo mwezi Aprili, baada ya mkandarasi kubainika kubomoa jengo lote licha ya agizo hilo.

Profesa Mshiriki wa Sayansi ya Moto katika Chuo cha John Jay, Glenn Corbett, amesema uchimbaji wa kina karibu na jengo lililokuwepo unaweza kusababisha kuyumba kwa misingi ya jengo hilo endapo tahadhari na hatua stahiki za kiusalama hazitachukuliwa.
Meya wa New York, Zohran Mamdani, amesema timu za uokoaji zinaendelea kufanya kazi katika mazingira hatarishi, huku akieleza kuwa juhudi hizo zinaweza kuchukua siku kadhaa kutokana na ukubwa wa eneo lililoporomoka.

Miongoni mwa manusura ni mwanamke aliyekuwa na ujauzito wa wiki sita, ambaye aliokolewa akiwa hai kutoka chini ya vifusi. Pia, mkazi mmoja aliyekuwa amenaswa aliweza kuwasiliana na waokoaji kabla ya kutolewa akiwa hai.
Aidha, familia kadhaa zimeathirika, zikiwemo za watoto wawili wenye umri wa miaka miwili na saba ambao walinaswa pamoja na mama yao, lakini baadaye waliokolewa wakiwa hai.

Wakazi wapatao 40 waliopoteza makazi yao wamepata hifadhi ya muda katika kituo cha YMCA kilichopo karibu na eneo la tukio.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mashtaka wa Brooklyn, Eric Gonzalez, amesema ofisi yake inashirikiana na mamlaka za ujenzi pamoja na vyombo vya usalama kuchunguza iwapo kulikuwa na uzembe au vitendo vya jinai vilivyochangia kutokea kwa ajali hiyo.
Mamlaka zimeagiza kusimamishwa kwa shughuli zote za ujenzi katika eneo jirani na kuwataka wananchi kuepuka eneo la tukio wakati operesheni za uokoaji na uchunguzi zikiendelea.


