×

NRM Yakataa Pendekezo la Muhoozi Kurithi Urais wa Museveni

Chama tawala nchini Uganda, National Resistance Movement (NRM), kimepinga pendekezo la kumuidhinisha Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa Rais Yoweri Museveni, kuwa mrithi wa kisiasa wa baba yake na mgombea wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2031.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Shirika la Habari la AFP, baadhi ya wajumbe wa kamati kuu ya utendaji ya chama hicho walipinga mpango huo katika mkutano wa faragha uliofanyika Jumanne, Novemba 10, 2026, uliojadili suala la urithi wa uongozi wa Rais Museveni.

Katika mkutano huo, wajumbe walijadili uwezekano wa kumpitisha Muhoozi, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Majeshi ya Uganda, kuwa mgombea wa urais wa chama hicho katika uchaguzi ujao.

Hata hivyo, zoezi la upigaji kura kuhusu pendekezo hilo lilisitishwa baada ya baadhi ya wajumbe kuibua upinzani mkali. Vyanzo vilivyonukuliwa na AFP vimedai kuwa wajumbe wanne walikuwa wameunga mkono pendekezo hilo huku watatu wakilipinga kabla ya zoezi hilo kusitishwa.

Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 82, ameiongoza Uganda tangu mwaka 1986, huku mwanawe Muhoozi Kainerugaba, mwenye umri wa miaka 52, akizidi kujitokeza katika medani za kisiasa na kuashiria nia yake ya kuwania urais mwaka 2031.

Hata hivyo, matarajio ya Muhoozi yameendelea kuibua mjadala na wasiwasi ndani ya chama tawala, hasa kutokana na mwenendo wake wa kisiasa na jumbe zenye utata ambazo amekuwa akichapisha kwenye mitandao ya kijamii.

Chanzo kimoja ndani ya NRM kimeeleza kuwa baadhi ya wanachama hawana uhakika na uwezo wake wa kuongoza kutokana na kile kilichoelezwa kuwa mtindo wake wa kukabiliana na wakosoaji kwa ukali.

Aidha, chanzo kingine kimesema Museveni amekuwa akishauriwa kumuondoa mwanawe katika jeshi na kumpa nafasi ya kiraia ili apate fursa ya kuelewa changamoto za wananchi na kujiandaa kwa majukumu ya uongozi wa nchi.

Suala la nani atamrithi Museveni lilianza kujadiliwa kwa uzito zaidi mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, baada ya rais huyo kukutana na viongozi wakuu wa NRM na kuwasilisha waraka ulioeleza kuwa mwanawe ana sifa zinazohitajika kuiongoza Uganda.

Upinzani uliojitokeza ndani ya NRM unaashiria kuwa mpango wa Muhoozi kurithi nafasi ya kisiasa ya baba yake bado haujapata uungwaji mkono wa pamoja ndani ya chama hicho, huku mjadala kuhusu mustakabali wa uongozi wa Uganda ukiendelea kushika kasi.

Leave a Comment