×

Tanzania Yajibu Kauli Ya Uingereza Kuhusu Hukumu ya Tundu Lissu

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetoa tamko kuhusu kauli iliyotolewa na Waziri wa Afrika na Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Kirsty McNeill, kufuatia kutiwa hatiani kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, na Mahakama yenye mamlaka nchini Tanzania.

Katika taarifa iliyotolewa Novemba 12, 2026, jijini Dodoma, Wizara hiyo imesema imepokea na kuzingatia tamko la Waziri huyo wa Uingereza kuhusu hukumu ya Lissu, huku ikisisitiza kuwa suala hilo lilishughulikiwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wizara imeeleza kuwa mchakato wa kisheria ulizingatia taratibu za haki, ikiwemo haki ya mtuhumiwa kupata uwakilishi wa kisheria na kusikilizwa kwa haki. Aidha, imeeleza kuwa Lissu alifafanuliwa kikamilifu kuhusu haki yake ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Katika taarifa hiyo, Serikali imesisitiza kuwa uhuru wa Mahakama ni nguzo muhimu ya mfumo wa kikatiba nchini na kutoa wito kwa washirika wote wa kimataifa kuheshimu uhuru wa Mahakama pamoja na taratibu za kisheria zinazotumika nchini.

Pamoja na msimamo huo, Wizara imesema Serikali ya Tanzania inaendelea kujikita katika kulinda haki za binadamu na utawala wa sheria.

Aidha, Serikali imeeleza kuwa Tanzania na Uingereza zina uhusiano wa kihistoria na wa kirafiki uliojengwa kwa misingi ya kuheshimiana, ushirikiano wa maendeleo, biashara, uwekezaji, elimu na mahusiano ya wananchi wa nchi hizo mbili.

Imesisitiza kuwa masuala yenye maslahi kwa pande zote yanapaswa kushughulikiwa kupitia mazungumzo ya kidiplomasia yenye kujenga, kuheshimiana na kuepuka kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine.

Leave a Comment