
KILIMANJARO, 12 Novemba 2026: Kampuni ya Ahsante Tours imefanikiwa kuratibu safari ya Kili Insurance Summit 2026, kwa kuwaongoza na kuwasaidia jumla ya washiriki 22 kutoka ARiS Risk & Insurance Solutions Limited na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro na kurejea salama.
Safari hiyo ilianza tarehe 6 Novemba kupitia lango la Machame, ambapo washiriki wote 22 walifanikiwa kufika kilele cha Uhuru, sehemu ya juu zaidi barani Afrika yenye urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari, tarehe 11 Novemba. Washiriki walikamilisha safari yao ya kushuka mlimani kupitia lango la Mweka tarehe 12 Novemba 2026.

Kama mshirika mkuu wa uongozi na uratibu wa safari hiyo, Ahsante Tours ilikuwa na jukumu muhimu katika kuratibu safari nzima, kuanzia maandalizi ya awali hadi washiriki walipomaliza kushuka mlimani. Majukumu hayo yalijumuisha kusaidia maandalizi ya kimwili ya washiriki, kuandaa mazoezi ya mafunzo, kuratibu mahitaji ya safari ya kupanda mlima pamoja na kutoa mwongozo na usaidizi katika kila hatua ya safari.
Kabla ya safari hiyo, washiriki walishiriki katika mazoezi ya viungo yaliyofanyika Pugu, Dar es Salaam, yakifuatiwa na safari ya siku mbili ya matembezi ya milimani katika Milima ya Uluguru, Morogoro. Mazoezi hayo yalilenga kuwaandaa washiriki kukabiliana na changamoto za kimwili za kupanda Mlima Kilimanjaro.

Akizungumzia mafanikio ya safari hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Ahsante Tours, Cuthbert Swai, alisema:
“Kufanikiwa kuwaongoza wapandaji 22 kufika kileleni na kurejea salama ni mafanikio makubwa. Hili limewezekana kupitia maandalizi mazuri, ushirikiano na uratibu katika kila hatua ya safari. Tunajivunia kuwa sehemu ya safari hii na tunawashukuru wote waliochangia kufanikisha zoezi hili.”
Safari hiyo iliyobeba kaulimbiu ya “Miaka 30 ya Ubora katika Sekta ya Bima, Tukifikia Mafanikio Mapya kwa Pamoja,”* ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya mageuzi katika soko la bima nchini Tanzania.

Zaidi ya changamoto ya kupanda mlima, safari hii imebeba ujumbe kwamba mafanikio huanza muda mrefu kabla ya kuanza safari yenyewe. Kupitia dhana ya kampeni isemayo “Safari ya Kufika Kileleni Haianzi Mlimani,” mpango huu unaonesha umuhimu wa maandalizi, kutambua vihatarishi mapema na kuchukua hatua sahihi za kuvidhibiti.
Kanuni hizi zinaendana na namna Ahsante Tours inavyoratibu safari za kupanda milima, ambapo mipango madhubuti, waongozaji wenye uzoefu, ushirikiano na kuzingatia mahitaji ya washiriki ni mambo muhimu katika kuhakikisha safari inakuwa salama na yenye mafanikio.
Kukamilika kwa mafanikio kwa safari hii ni hatua muhimu na kumbukumbu ya pekee kwa washiriki wote. Pia, kunaonesha kile kinachoweza kufikiwa kupitia maandalizi, ushirikiano na dhamira ya pamoja ya kufikia mafanikio mapya.
