
Kikundi cha wasanii cha Ajabu Ajabu kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), kimezindua mradi wa ‘Ahaa Niiambie’ unaolenga kukuza ubunifu, vipaji na kuimarisha uandaaji wa filamu zenye kuonesha uhalisia wa maisha ya Mtanzania.
Mradi huo unalenga kuwapa nafasi wasanii na wabunifu kuibua simulizi za asili zinazotokana na maisha, tamaduni na mazingira ya Watanzania, ambazo hazijapata nafasi ya kuwasilishwa kupitia sanaa ya filamu.

Kupitia mradi huo, washiriki wanatakiwa kuandaa filamu fupi ya sekunde 90, ambapo kazi zitakazofanya vizuri zitafanyiwa tathmini na washiriki 12 watakaochaguliwa kupata mafunzo maalumu ya siku 10 kuanzia Novemba 19 hadi 28, 2026, kwa ajili ya kuendeleza uwezo wao katika utengenezaji wa filamu.
Akizungumzia mradi huo, Jesse Gerald Mpango, ambaye ni mwanzilishi wa kikundi cha Ajabu Ajabu, amesema lengo kubwa ni kuibua simulizi asilia ambazo hazijapata nafasi ya kuonekana au kusikika, huku akiamini kuwa Tanzania ina hadithi nyingi zinazostahili kuwasilishwa kupitia filamu.

Kwa upande wake, Getrude Malizeni, mwandishi wa filamu na mmoja wa waanzilishi wa Ajabu Ajabu, amesema sehemu kubwa ya filamu zinazozalishwa nchini zimekosa uhalisia kutokana na tabia ya baadhi ya watengenezaji kuiga kazi za wengine badala ya kuibua mawazo yanayotokana na mazingira yao.
Amesema kupitia mradi wa ‘Ahaa Niiambie’, wanakusudia kuchochea utengenezaji wa filamu zinazobeba utambulisho wa Kitanzania na Kiafrika, huku zikionesha maisha halisi ya jamii.

Naye Paulo Juma Iddy, ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki wa uzinduzi huo, amesema mradi huo ni fursa muhimu kwa wasanii kujifunza, kuendeleza vipaji vyao na kupata uzoefu zaidi katika tasnia ya filamu.
Mradi huo unatarajiwa kuwa jukwaa la kuibua vipaji vipya na kuwapa nafasi wabunifu wa Tanzania kuwasilisha simulizi zao kwa njia ya kisanii, huku ukisisitiza umuhimu wa kuwa na filamu zenye utambulisho na uhalisia wa jamii ya Kitanzania.