×

Vodacom Foundation Yakabidhi Jengo la Kituo cha Rasilimali za Walimu Mbezi

Vodacom Tanzania Foundation imefanya maboresho ya Kituo cha Rasilimali za Walimu (TRC) katika Shule ya Msingi na Ufundi Mbezi, Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kupitia teknolojia.

Kituo hicho kimezinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ambaye amekata utepe kuashiria kukamilika kwa maboresho ya jengo hilo.

Sambamba na uzinduzi huo, Vodacom Tanzania Foundation imekabidhi vifaa mbalimbali vya kisasa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), vikiwemo kompyuta 30 zilizounganishwa na intaneti, UPS 30, meza na viti 30, televisheni yenye ukubwa wa inchi 75 pamoja na madawati 90 kwa ajili ya wanafunzi.

Makabidhiano ya vifaa hivyo yamefanywa na Mkuu wa Idara ya Uendelevu na Ubia wa Vodacom Tanzania Foundation, Pauline Koola, huku yakishuhudiwa na Meneja Mauzo wa Vodacom Tanzania eneo la Kibaha, Fadhili Linga, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi, Lois Bawazir Hassani, pamoja na mwakilishi wa Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Ubungo, Hamida Semkuya.

Maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, kuwawezesha walimu kupata maarifa kupitia teknolojia na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika sekta ya elimu.

Aidha, uwepo wa kompyuta zilizounganishwa na intaneti unatoa fursa kwa walimu kutumia rasilimali za kidijitali katika kuboresha mbinu za ufundishaji na kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu.

Leave a Comment