
Jeshi la Ukraine limedai kwamba wanajeshi wan chi jirani la Belarus, wamevuka mipaka wakiwa na vifaru na silaha nyingine nzito na kuingia nchini Ukraine kwa lengo la kwenda kuisaidia Urusi.
Taarifa hizo zinakuja saa chache baada ya Serikali ya Marekani kueleza kwamba inazo taarifa za kiintelijensia zinazoonesha kwamba Belarus inajiandaa kuvuka mpaka na kuingia nchini Ukraine kuisaidia Urusi.
Tangu kuanza kwa mzozo baina ya Ukraine na Belarus, rais wa nchi hiyo, Alexander Lukashenko ambaye ni swahiba mkubwa wa Rais Vladimir Putin wa Urusi, alitangaza kwamba nchi yake ipo tayari kuisaidia Urusi katika uvamizi wake nchini Ukraine.
Kuingia kwa majeshi ya Belarus nchini Ukraine, kunatajwa kuwa kutazidi kuifanya vita hiyo kuzidi kuwa mbaya zaidi.
Hapo jana, mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Urusi na Ukraine yaliyofanyika karibu na mpaka wa Belarus, yalishindwa kuzaa matunda baada ya pande hizo mbili kutofikia muafaka wa kusimamisha mapigano.