
Waziri wa Afya, Mohamed Omary Mchengerwa, amewapongeza watumishi wanne wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam kwa kuokoa maisha ya mama na mtoto aliyefikishwa hospitalini hapo akiwa katika hali mahututi wakati wa kujifungua.
Tukio hilo lilitokea Novemba 13, 2026, ambapo mama huyo alifika hospitalini hapo akiwa amezidiwa na hali yake kuhitaji msaada wa haraka wa kitabibu ili aweze kujifungua salama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya, watumishi hao walimkimbilia mama huyo na kumsaidia haraka, hatua iliyowezesha kuokoa maisha yake pamoja na ya mtoto aliyekuwa tumboni.
Watumishi waliotajwa kuhusika katika tukio hilo ni Bi. Jestina Mahenge, Muuguzi; Bi. Saada Ramadhani, Afisa Muuguzi Msaidizi; Bi. Hamisa Daud, Mhudumu wa Afya; na Bi. Rukia Juma, Mlinzi.
Kutokana na hatua hiyo, Waziri Mchengerwa amewapongeza watumishi hao na kuwazawadia Shilingi 500,000 kila mmoja kama ishara ya kutambua mchango wao katika kuokoa maisha ya wananchi.
Aidha, amewataka watumishi wote wa afya nchini kuendelea kufanya kazi kwa weledi, kujitolea na moyo wa kuwahudumia wananchi wakati wote, hata katika mazingira yasiyotabirika.
